Tuesday, July 12, 2016

MIMBA ZINAZOYEYUKA, ZINAZOGEUKA JIWE

lithopedion effect

Wapo baadhi ya wanawake ambao wamewahi kupata dalili na viashiria vya ujauzito pamoja na kupimwa kipimo cha mkojo na kuthibitishiwa kuwa wana ujauzito lakini baadaye wakabaini kuwa ujauzito haupo tena.

Katika hali ya namna hii mawazo ya watu wengi mara moja huamini kuwa wamerogwa na hawana fikira au mawazo mbadala ya kuelezea chanzo cha tatizo hilo.

Wengi hukimbilia kwa waganga wa tiba za jadi na kutumia mitishamba kwa lengo la kurejesha ujauzito na kutumia fedha za rasilimali zao bila mafanikio.

Wengine huenda katika nyumba za ibada ili kufanyiwa maombi kwa Imani kuwa hali hiyo inatokana na nguvu za giza. 
Baadhi ya watu wanaosimulia au kusimuliwa kuhusu visa vya namna hii, nao huwa wanaamini kuwa hayo ni maajabu na wanaishia kukumbuka msemo wa Kiswahili usemao “ukistaajabu ya Musa, utayaona ya Firauni.”

Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Ngeme Makala katika wilaya ya Bunda mkoani Mara, ambaye aliripotiwa na vyombo vya habari mwaka 2011 kuwa alipata tatizo hili alisema:
“tukio la kwanza ambalo lilianza kunishangaza ni baada ya ujauzito wangu kufikisha miezi sita kwani ulipotea ghafla na kuzua maswali mengi kwa watu, akiwamo mume wangu.  Kufuatia hali hiyo, mume wangu alinipeleka kwa bibi mmoja ambaye baada ya kumweleza tatizo alinipa dawa za mitishamba.”

Jambo hili ingawa linaweza kuonekana kama maajabu, miujiza, kurogwa au jambo la kushtusha, lakini sayansi inaweza kutupatia maelezo ya kina kuhusu nini chanzo cha tatizo hilo la afya ya uzazi.
Wanasayansi wanasema kuwa hali hii hutokea mara nyingi pale mimba inapotunga nje ya mfuko wa uzazi na mtoto kufariki akiwa tumboni.  Mtoto anaweza kufariki wakati mimba inapofikisha umri wa majuma 14 (miezi 3 na nusu) na kuendelea, umri ambao mwili wa mama hauwezi tena kusharabu tena kiumbe kilichokufa.

Baada ya hapo, mwili wa mtoto hukauka na kuwa mgumu kama jiwe kiasi kwamba hauwezi kushambuliwa na bakteria au kuoza kutokana na ukweli wa kisayansi kuwa kiumbe hicho huwa na madini ya kalisi ambayo hupatikana katika mifupa.

Hali hii ya kiumbe kukauka na kuwa katika hali ya ugumu kama jiwe hutokana na mchakato ambao kwa lugha ya kitaalamu hujulikana kama “calcification” kwa sababu mifupa ya mtoto aliyekauka tumboni inaganda, kukauka na kuwa migumu kutokana na madini ya kalisi.

Mmoja wa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake nchini, Dk Onesmo Rwakyendera amewahi kuilezea hali ya mimba zinazopotelea tumboni na kukauka kama jiwe kwa kusema: “Hawa huitwa “Mummies” na kutokana na jina hili, watoto wanapokufa tumboni wakagandishwa na dawa Fulani, hali hiyo huitwa “mummifying process” na baadaye hutoka na mama akadhani amejifungua jiwe.”

Kitaalamu hali hii hujulikana kama Lithopedia au ‘mimba ya mtoto jiwe.’  Ushahidi wa watafiti wa maswala ya historia ya utabibu wanabainisha kuwa kwa mara ya kwanza hali ya mimba kupotelea tumboni ilielezewa na Dk Abu al-Qasim Khalaf ibn al-Abbas Al-Zahrawi maarufu kama Albucasis katika karne ya 10.  Hata hivyo,watafiti wanadai kuwa katika miaka 400 ya ukusanyaji na maandiko na tafiti za kitabibu ni visa vichache visivyozidi 300 ambavyo vimeandikwa kuhusu hali hii.

Kisa cha kale zaidi kuhusiana na hali hii ni kile kilichogunduliwa mwaka 1990 na profesa Leland Bement wa chuo kikuu cha Texas katika uchimbaji wa mabaki ya kale.  Baada ya wataalamu wa elimu ya mabaki ya kale Christine na mwenzake Bruce Rothschild kufanya utafiti na uchunguzi wa kina walibaini kuwa kisa hicho kilitokea miaka 3,100 iliyopita huko Texas, Marekani.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa mwaka 2007 katika jarida la kitabibu lijulikanalo kama Singapore Medical Journal toleo namba 48(9), mimba zinazotunga nje ya kizazi ni chache sana kiasi kwamba kati ya mimba 11,000 ni moja tu inaweza kutunga katika eneo hilo.  Na kati ya mimba zinazotunga nje ya kizazi ni asilimia moja hadi mbili ya mimba zote zinazoweza kupotelea tumboni na kuwa ‘mtoto jiwe’.

Taarifa za kitabibu toka pande mbalimbali za dunia zinaonyesha kwamba baadhi ya wanawake wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la mimba kupotelea tumboni na baadaye kugunduliwa kuwa wana ‘mtoto jiwe’ baada ya miaka mingi.  Visa vya namna hii vimeripotiwa Nicaragua, Brazil, Colombia, Chile, Africa Kusini, Morocco, Ghana, DR Congo, Thailand, Korea Kusini, India na kwingineko.

Mwaka 2013 vyombo mbalimbali vya habari viliripoti kuhusu Huang Yijun, kikongwe wa miaka 92 mwenyeji wa China ambaye mimba yake ilipotelea tumboni na ikaja kugundulika miaka 60 baada ya mtoto kufia tumboni na akakauka hadi kuwa mgumu kama jiwe.  Hivi karibuni vyombo vya habari vimeripoti kisa cha Estela Melendez, kikongwe mwenye miaka 90, mkazi wa San Antonio nchini Chile, ambaye alipata mimba mwaka 1965 na ikapotelea tumboni hadi ilipogunduliwa mwaka jana baada ya miaka 50.  Mimba hii iligunduliwa baada ya kupigwa picha ya X-ray kwa ajili ya matatizo mengine ya kiafya yaliyompeleka hospitalini kupata huduma za kitabibu.

Katika nchi zinazoendelea hasa maeneo ya vijijini barani Africa, ambako huduma za afya ya uzazi ni duni kutokana na ukosefu wa vifaa na vitenganishi vya kisasa vya ugunduzi wa matatizo ya afya ya uzazi, wanawake wengi wenye hali hii hawagunduliki.  Na wengine kutokana na imani za jadi zilizoota mizizi, wanapoona hali ya kupotea kwa dalili na viashiria vya ujauzito, hutafuta huduma za afya kwa wataalamu wa tiba za jadi na wapiga ramli ambako huambiwa kuwa wamerogwa.


Hali ya namna huleta taharuki, hofu na tashtiti katika jamii na mwishowe huwa chanzo cha visasi na mauaji ya kinyama yasiyokuwa na msingi wowote.  Kutokana na ukweli na ushahidi wa kisayansi wa chanzo cha hali ya mimba kupotelea tumboni ni busara kwa mwanamke mwenye dalili hizi akichukua hatua za maksudi kuwaona madaktari ili kupata ushauri wa kitaalamu badala ya kukimbilia kwa waganga wa jadi akiamini kuwa amerogwa.
Share:

No comments:

Post a Comment