Vichocheo vya jinsi ni homoni zinazohusiana na mabadiliko ya
ukuzi ya wanaume na wanawake wanapofikia umri wa kuzaa.
Homoni hizi kwa wanaume huwezesha uzalishaji wa tezi
zinazotengeneza mbegu za kiume na kwa wanawake mayai. Kuna aina mbalimbali za vichocheo vya jinsi
kama vile testosterone, progesterone, stradiol, inhibin B, activin na homoni
zijulikanazo kama antimullerian (AMH).
Wanaume
Kwa upande wa wanaume upungufu wa vichocheo vya jinsi
unahusiana kwa kiasi kikubwa na upungufu wa homoni ya testerone. Na kwa wanawake tatizo hili hujitokeza zaidi
pale homoni ya progesterone inapopungua mwilini.
Upungufu wa vichocheo vya jinsi ni tatizo linaloweza
kuathiri vibaya hali ya ubora wa maisha, hasa kwa wanandoa.
Mbali na matatizo ya kiafya, upungufu
huu unaweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa na kusambaratika kwa familia.
Ni muhimu pia kutambua kuwa tatizo hili pia kwa namna moja
ama nyingine linaathiri kazi za ubongo, mishipa ya damu, afya ya moyo, afya ya
mifupa na mchakato wa kikemikali unaosaidia mwili kuendeleza utendaji mzuri wa
seli zake.
Wanaume wenye upungufu wa vichocheo vya jinsi wanaweza kupata
matatizo ya kupungukiwa hamu ya tendo la ndoa, upungufu wa nguvu za kiume,
kushindwa kutungisha mimba, kupungua kwa ukubwa wa misuli ya mwili na kupotea
kwa tabia za kiume.
Matatizo mengine ni uchovu wa mwili, udhaifu wa mifupa na
matiti kuwa makubwa. Mara nyingi chanzo
cha tatizo hili kwa wanaume ni maradhi yanayoathiri korodani, sehemu ya ubongo
ijulikanayo kama hypothalamus na tezi ya pituitary. Matibabu ya saratani na mionzi pia ni mambo
mengine yanayosababisha tatizo hili.
Umri mkubwa nao unachangia kutokea kwa tatizo hili. Chama cha Wataalamu wa Vichocheo Mwilini cha
Marekani (American Association of Clinical Endocrinologys) katika utafiti wake
uliochapishwa mwaka 2001 katika jarida liitwalo Jornal of Clinical
Endocrinology & Metabilism, toleo namba 86, kinadai kuwa wanaume wenye umri
zaidi ya miaka 75 kufikia kiasi cha asilimia 30 wana upungufu wa vichocheo vya
jinsi.
Mambo mengine yanayoweza kuchangia kutokea kwa tatizo hili
ni pamoja na maradhi ya kuambukiza kama vile Kifua Kikuu (TB), Ukimwi na
uambukizo wa virusi vinavyosababisha uvimbe wa tezi za mate (mumps). Unene wa kupindukia na matumizi holela ya
dawa zenye homoni pia ni mambo mengine yanayochangia.
Wanawake
Kwa wanawake, upungufu wa vichocheo vya jinsi unaweza
kusababisha hali ya mwili kuchoka mara kwa mara, upungufu wa hamu ya tendo la
ndoa, msongo wa mawazo, wasiwasi, hali ya kushindwa kuzingatia mambo na kukosa
usingizi. Matatizo mengine ni nywele
kunyonyoka, udhaifu wa mifupa na kuvurugika kwa mtiririko wa siku za hedhi.
Utafiti wa hivi karibiuni unaonyesha kuwa watu wengi
wanaokabiliwa na tatizo la upungufu wa vichocheo vya jinsi mwilini, chanzo ni
kemikali zinazopatikana katika bidhaa za matumizi nyumbani kama vile shampoo,
baadhi ya sabuni za unga, rangi za kucha, spray za nywele na vifungashio vya
plastiki.
Utafiti huo unaonesha kuwa, bidhaa zenye kemikali ya phthalates,
ambayo inaongezwa katika vifungashio na bidhaa za plastiki ili kuongeza uangavu
na uwezo wa kukunjika kwake zinachangia kwa kiasi Fulani kutokea kwa tatizo
hili.
“Tulipata ushahidi kuwa kupungua kwa kiasi cha homoni ya
testosterone ndani ya damu kuna uhusiano na ongezeko la watu kugusana na
kemikali ya phthalate, hali hii inahusisha wavulana na wasichana wenye miaka sita hadi
12, na wanaume na wanawake wenye miaka 40 hadi 60,” anasema Dk John D. Meeker
wa Chuo Kikuu cha Michigan, mmoja wa viongozi wa utafiti huo.
Kutokana na kuongezeka kwa matangazo ya waganga wa jadi
wanaotibu tatizo la nguvu za kiume hapa nchini, hii ni ishara kuwa kuna
ongezeko kubwa la matatizo ya upungufu wa vichocheo vya jinsi katika jamii.
Jamii inashauriwa kutafuta huduma za kitabibu zenye ushahidi
kisayansi ili kukadiria tatizo hili. Ili
kupunguza hatari ya kupata tatizo hili ni busara kujiepusha na matumizi holela
ya dawa za hospitalini na vipodozi ambavyo vimepigwa marufuku na Serikali.
Homoni ni kichocheo kinachozalishwa ndani ya kiumbe hai na
kusafiri kupitia vimiminika ndani ya mwili kama vile damu kwa ajili ya
kuchokoza au kuhamasisha tishu au seli
Fulani zifanye jambo Fulani.
Zipo aina nyingi za homoni kama vile kuendeleza ukuaji,
umeng’enyaji wa vyakula, kufanikisha tendo la ndoa, kudhibiti joto la mwili na
kutoa taarifa ya ukosefu wa maji mwilini kwa kupata kiu.
Homoni huzalishwa kwenye tezi maalumu ndani ya mwili kama
vile kwenye ubongo, shingo, ini, kende kwa upande wa wanaume na ovary kwa
wanawake.
Wataalamu wanasema homoni inatolewa kwa kiwango
kidogo sana, lakini huweza kutoa amri kwa haraka sana ili kufanikisha jambo
Fulani la mwili.
No comments:
Post a Comment