Wednesday, July 20, 2016

NI HATARI KWA MWENYE VVU KUNENEPA SANA


Mtu mmoja alisema kuwa alielimishwa na wataalamu wa afya kwamba anayeishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) anapaswa kula vizuri ili afya yake iimarike.  Pia amekuwa akisikia kwa watu ni vizuri mwenye VVU akawa mnene ili kuwa na nguvu ya kukabiliana na virusi.  Lakini upande mwingine wa shilingi watu wanapiga vita unene kwa kuwa ni hatari kwa afya.  Kwa sababu hiyo akataka kuelimishwa kwa kuuliza: “Je uzito kupita kiasi una madhara yoyote kwa mtu anayeishi na VVU?”

Miongo miwili iliyopita mtu aliyepata virusi vya ukimwi (HIV) alitambulika zaidi kwa kupoteza uzito na kukonda, na hivyo alionekana kama ndio mwisho wa maisha yake.


Siku hizi mtu anayeishi na VVU hakatiwi tamaa na anajulikana kuwa ana ugojwa sugu, na mara nyingi anaongezeka uzito na unene kama vile mtu asiyekuwa na maradhi yoyote.

Kwa kiasi kikubwa mafanikio haya yanatokana na matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs), kufanya mazoezi na lishe bora.

Katika ngazi ya dunia, tafiti bado zinaendelea ili kubainisha kwa uhakika athari mbaya ya kuongezeka uzito na unene kupita kiasi kwa watu wanaoishi na VVU na wagonjwa wa Ukimwi.

Athari hizi zikijulikana zitasaidia kubuni njia za namna bora ya kudhibiti uzito na unene kupita kiasi kwa watu wazima wanaoishi na virusi vya Ukimwi.  Hapa Tanzania kuna haja kubwa ya kufanya utafiti zaidi ili kuona uhusiano wa matumizi ya ARVs na kuongezeka kwa uzito na unene kupita kiasi.

Tafiti hizo zitasaidia kujibu maswali ya wananchi kwa ushahidi wa kisayansi na kuandaa mwongozo wa namna ya kupunguza uzito na unene kupita kiasi kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
Kwa kiasi kikubwa, unene na uzito kupita kiasi unasababishwa na mtu kukosa kufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho, kuvuta sigara, kunywa pombe kwa wingi na ulaji usiofaa.  Urithi kutoka kwa wazazi nao unachangia kwa baadhi ya watu kuwa na uzito au unene kupita kiasi.

Ulaji usiofaa ni pamoja na kula kwa wingi vyakula vya wanga na vyenye mafuta au sukari nyingi, na kula kiasi kidogo vyakula vyenye nyuzi lishe kama vile mboga za majani na matunda.

Zaidi ya hayo, watu wenye nguvu ya kiuchumi, wanaotumia vyombo vya usafiri, wanaofanya kazi za ofisini au dukani, wasiokuwa na taarifa za kutosha kuhusu afya na lishe, wenye msongo wa mawazo na wanaofuata marafiki wasiojali afya zao wako katika hatari kubwa zaidi ya kuwa wanene na wazito kupita kiasi.

Unene na uzito kupita kiasi ni jambo la hatari zaidi kiafya kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.  Kwa sababu watu wanene na wenye uzito mkubwa  wako katika hatari ya kupata magonjwa ya aina mbalimbali kama vile shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari aina ya pili, miguu kuuma na kuvunjika mifupa.

Ni wazi kuwa mtu anayeishi na virusi vya Ukimwi akiwa na mzigo wa magonjwa mengine kinga yake itapungua zaidi na mwili utachoka kwa haraka na hiyo ni hatari sana kwa mtu huyo.

Dawa za ARVs pia zinaweza kuongeza unene na uzito kupita kiasi kwa mtumiaji hata akizitumia kwa usahihi.  Kama hali hiyo itatokea, mgonjwa anashauriwa arudi katika kliniki yake haraka ili apate ushauri.

Mtu anayeishi na virusi vya ukimwi ale mlo kamili, afanye mazoezi, apunguze mawazo, aache kunywa pombe na kuvuta sigara, apate muda wa kutosha wa kulala, na azidi kujielimisha na kuhudhuria kliniki kama alivyopangiwa.
Share:

No comments:

Post a Comment