Wapo watu wana harufu mbaya ya kinywa kiasi cha kukosa amani
mbele ya hadhara. Hawa ni wale
wanaotambua juu ya tatizo hilo. Wengine hawaelewi
lakini huwa kero kwa jamaa zao wanaolazimika kuwa wavumilivu ili kutoharibu
uhusiano uliopo.
Harufu mbaya ya kinywa inaweza kuwa tatizo linalokukera hata
kukusababishia wasiwasi unapojumuika na wenzako katika masuala mbalimbali, iwe
ofisini au mtaani.
Kitu ambacho wengi hawafahamu ni kwamba dawa nyingi zinazouzwa
na kuelezwa kutibu tatizo hilo hazina uwezo wa kuleta suluhu ya kudumu bali ya
muda mfupi tu. Dawa hizo hazitibu tatizo
bali linagusa tu athari zake.
Usishangae kwa sababu ya uwapo wa dawa kadha wa kadha
zilizotengezwa kwa ajili ya kupambana na harufu ya kinywa. Dawa hizi hazijaelekezwa kwenye kiini cha
tatizo bali linapoishia.
Ili kumaliza harufu ya kinywa ni lazima kujua imesababishwa
na nini ambacho kitadhibitiwa kikamilifu ili kupata suluhu ya kudumu. Zipo sababu nyingi zinazochangia harufu hii.
Baadhi ya vyakula, magonjwa au tabia huweza kusababisha
harufu mbaya ya kinywa. Pamoja na hayo
habari njema ni kwamba unaweza kuondokana na kadhia hiyo kwa kufanya usafi
madhubuti wa kinywa chako.
Ili kukabiliana na tatizo hili inashauriwa kuwa macho wakati
wote. Hili litafanikiwa endapo
utazifahamu dalili za kuwa na harufu isiyopendeza kutoka kinywani mwako. Lakini ni muhimu kufahamu kwamba harufu mbaya
hutofautiana kutegemea chanzo.
Kuna baadhi ya watu wana mashaka na harufu ya vinywa vyao
hata kama wana tatizo wakati wapo wenye harufu mbaya ila hawajitambui.
Kwa sababu ni vigumu kutathmini harufu ya kinywa chako
mwenyewe, unaweza kumuuliza mtu wako wa karibu ili kujiridhisha kama una harufu
mbaya ya kinywa.
Ukithibitisha kuwa nayo, ni vyema ukapitia ufanyaji wako wa
usafi wa kinywa. Jaribu kufanya
mabadiliko ya mfumo wa maisha kama vile kupiga mswaki mara baada ya kula na
kunywa maji mengi.
Ukiona tatizo linaendelea licha ya kufanya mabadiliko haya,
ni vyema ukamuona daktari wa kinywa na meno kwa msaada zaidi.
Ni daktari huyu pekee anapaswa kukueleza
chanzo cha tatizo hilo ambalo mara nyingi huwa linatokana na matatizo yaliyomo
kinywani.
Uchunguzi wa daktari wa kinywa na meno unaweza ukakupeleka
kwa madaktari wengine kwa uchunguzi zaidi kama ataona tatizo lako halitokani na
hali ya afya ya kinywa chako.
Sababu
Mara nyingi harufu mbaya ya kinywa huanzia mdomoni ingawa
vyanzo vyake ni vingi. Ugonjwa wa fizi
ni moja ya sababu ya harufu hii kwani husababisha kuvimba na kutoa damu wakati
wa kupiga mswaki, kung’ata kitu ama kutema mate.
Ugonjwa wa fizi hutokana na upigaji wa mswaki. Wakati mwingine huwa hauna maumivu kiasi
kwamba mtu anaweza kuwa nao na asijue.
Kutopiga mswaki ni sababu nyingine. Kama hupigi mswaki na kufanya flosi, mabaki
ya chakula yakikaa kwa muda huoza na kutoa harufu mbaya. Ulimi nao unastahili kufanyiwa usafi kwani
unafanana na taulo hivyo kushika mabaki ya chakula na kuweza kukaribisha bacteria
baada ya kula.
Meno ya Bandia
Meno ya bandia yasiyosafishwa mara kwa mara au ambayo
hayakai vizuri huweza kuhifadhi mabaki ya chakula na bacteria ambao kwa pamoja
huweza kuchangia kuwapo kwa harufu mbaya ya kinywa.
Meno Yaliyotoboka
Meno yaliyotoboka hayasafishiki unapopiga mswaki. Matundu yaliyopo kwenye meno hayo huweza
kuhifadhi chakula ambacho baada ya muda huoza na kutoa harufu mbaya.
Japokuwa tatizo hili husababishwa na meno yote yaliyotoboka,
lakini ya nyuma (magego) huchangia zaidi kwani mara nyingi watu wengi huwa
hawayasafishi. Hawafikishi mswaki kwenye
meno hayo.
Kinywa Kikavu
Kwa kawaida mate husaidia kusafisha kinywa na kuondoa mabaki
ya chakula hivyo mtu mwenye kinywa kikavu huweza kuwa na harufu mbaya kutokana
na upungufu huo.
Kwa kawaida kinywa kikavu hutokea usiku mtu anapolala na
akiamka huwa na harufu ya asubuhi ambayo huongezeka iwapo mtu huyo alilala
kinywa wazi. Hali hii pia huweza
kusababishwa na magonjwa ya tezi la mate matumizi ya baadhi ya dawa ambazo
huathiri ufanyaji kazi wa tezi la mate.
Dawa
Baadhi ya dawa zinachangia harufu mbaya ya kinywa endapo
zitasababisha ukavu wa kinywa. Lakini kuna
dawa nyingine zinapotumiwa kisha kumeng’enywa mwilini hutoa kemikali ambazo
humfanya mtumiaji atoe harufu yake wakati wa kupumua.
Maambukizi Kinywa
Harufu mbaya inaweza kusababishwa na maambukizi hasa kwenye
vidonda vilivyomo kinywani. Vidonda hivi
huweza kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kung’oa jino kisha pengo likapata
maambukizi.
Tumbaku
Uvutaji wa sigara au matumizi ya bidhaa zozote na tumbaku
mfano ugoro au shisha huambatana na harufu ambayo mara nyingi huwa mbaya. Wavutaji wa sigara wana uwezekano wa kupata
ugonjwa wa fizi ambao ni chanzo kingine cha harufu mbaya.
Vyakula
Kuna baadhi ya vyakula huleta harufu isiyo nzuri
kinywani. Vyakula kama vile vitunguu
maji, tangawizi na vinginevyo baada ya muda huleta harufu mbaya ya kinywa.
Magonjwa Mengine
Mara chache harufu mbaya ya kinywa huweza kusababishwa na
maambukizi sugu ya tezi (chronictonsilitis) ambayo bakteria wanaosababisha pia
huchangia harufu mbaya. Halikadhalika maambukizi
sugu kwenye pua na koo huweza kuchangia tatizo hili.
Saratani ya kinywa na koo na magonjwa yanayohusiana na mfumo
wa chakula pia huweza kusababisha harufu mbaya ya kinywa. Vilevile, kuna watu ambao hupata tatizo la
tindikali ya tumboni kuja kwenye koo na kinywani (gastroesophageal reflux
disease, GERD) nao wanaweza kupata tatizo hili.
Matibabu
Ili kuondokana na harufu mbaya ya kinywa, jikinge usipate
matundu kwenye meno na jizuie na magonjwa ya fizi kwa kufanya vizuri usafi wa
kinywa.
Kwa ujumla matibabu ya harufu mbaya ya kinywa hufanywa kwa
kuishughulikia sababu hiyo endapo daktari atagundua kuchangiwa na ugonjwa fulani
bado ataagiza utibiwe maradhi hayo kwanza.
Kuna mambo muhimu yanashauriwa ili kupunguza uwezekano wa
kuwa na harufu hii. Wataalamu wanaagiza
kupiga mswaki meno ulimi walau mara mbili kila siku, asubuhi baada ya kula na
usiku kabla ya kwenda kulala. Mara baada
ya kufanya hivyo, unapaswa kusukutua kwa dawa maalumu za kufanya hivyo
(mouthwash).
Fanya flosi angalau mara moja kwa siku huku ukinywa maji
mengi endapo una tatizo la kikavu kwani yanasaidia kupunguza tatizo hili.
Jitengenezee ratiba ya kumuona daktari wa kinywa
na meno.
Kumbuka kwa mtu wa kawaida
inampasa kumuona daktari wa kinywa na meno mara moja kila baada ya miezi sita,
yaani mara mbili kwa mwaka. Lakini mwenye
harufu mbaya unaweza kumuona mara nyingi zaidi na kufuata maelekezo yake.
Asante kwa elimu nzuri
ReplyDelete