Monday, November 21, 2016

MAZOEZI YANAEPUSHA MJAMZITO KUJIFUNGUA KWA UPASUAJI

mazoezi wakati wa ujauzito

Mara nyingi ujauzito huambatana na changamoto mbalimbali, ikiwamo kuumwa mara kwa mara hasa kwa kina mama ambao wanaishi katika mazingira magumu.  Pia, kuna kuugua kunakotokana na upungufu wa lishe.

Hata hivyo, licha ya wajawazito kushauriwa kutumia vyakula bora vyenye kila aina ya virutubisho kwa ajili yao na watoto wanaotarajia kuwaleta duniani, suala la mazoezi ni muhimu kwao.  

Utafiti unaonesha kwamba wanawake wanaofanya kazi nyingi ngumu katika kipindi cha miezi mitano ya mwanzo ya ujauzito wanakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujifungua salama.

Ingawa utafiti huo umebaini kwamba wajawazito hao wana fursa nzuri ya kujifungua salama, haina maana kwamba hawapaswi kutumia lishe inayotakiwa katika kipindi hicho.  Lishe bore katika kipindi cha ujauzito ni suala muhimu lisilohitaji mjadala ili kunusuru maisha ya mama na mtoto.

Kufanya kazi nyingi ngumu kunaweza kusababisha mjamzito kumfanya mtoto aliye tumboni kutonenepa kupita kiasi, hivyo kumsaidia mzazi kujifungua kwa urahisi na salama wakati unapowadia.

Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Granada cha Hispania unaonesha kuwa, pia wanawake wana fursa nzuri ya kutumia miezi minane ya ujauzito kufanya kazi nyingi bila kujali kwamba wako katika hali hiyo.

Mtafiti kiongozi wa utafiti huo, Dk. Jonatan Ruiz anasema wanawake wanaofanya mazoezi ya kutembea, kukimbia au kurukaruka mara kwa mara katika miezi minne ya mwanzo ya ujauzito wake katika mazingira mazuri ya kujifungua bila kufanyiwa upasuaji kwa kuwa watoto huwa na maumbo madogo.

Dk. Ruiz anasema hata wanawake wasiofanya mazoezi katika kipindi hicho, lakini wakaanza kufanya yale ya kutembea mara kwa mara, mara tatu kwa wiki wakati ujauzito unapokuwa mkubwa, wanaweza kukikwepa kwa urahisi ‘kisu’ siku ya kujifungua.

Anasema kutembea mara tatu kwa siku umbali wa kilometa tatu, kunasaidia kumfanya mtoto aliyeko tumboni asizubae au kulala lala, hali itakayoufanya mwili wake usinenepeane kwa kuwa naye atakuwa kama anafanya mazoezi.

Mtafiti huyo anasema, mtoto mchanga aliyeko tumboni anapotembezwa katika hali hiyo, misuli na ubongo wake huwa kazini muda wote hivyo hawezi kunenepa kiasi cha kumtesa aliyembeba tumboni.

Hata hivyo, Dk Ruiz anaongeza kuwa tatizo huja pale mama anapoamua kupumzika na mtoto humchukua muda mrefu kutulia tumboni kwa vile akili yake hufikiria kuwa anapaswa kuwa mazoezini muda huo.

“inaweza kuchukua hata saa mbili hivi tumboni (mtoto) anacheza cheza na utaratibu huo humtesa mama hasa kama amechoka anataka kupumzika kwa kulala,” anasema.

Utafiti huo umethibitisha kwamba watoto wanaozaliwa na kina mama wenye mazoezi ya aina hiyo, hupungua mara tatu zaidi tofauti na iwapo wazazi wao wasingefanya mazoezi hayo.

“kichanga kinapokuwa tumboni huanza kuwaza mambo fulani fulani ya kitoto na iwapo kitawaza kitapungua mwili kama ambavyo mtu mzima anavyowaza na kuwaza na hatimaye kupungua uzito au umbo,” anasema mtafiti huyo.

Dk Ruiz anasema kupungua kwa umbo la mtoto humsaidia mjamzito kutofanyiwa upasuaji kutokana na sababu mbili; kwanza sehemu zake za uzazi huwa zimepanuka kiasi cha kumudu kiumbe kutoka kwa urahisi na pili, mtoto anayetarajiwa kuzaliwa huwa na umbo linaloweza kumfanya atoke kwa urahisi.

Pia utafiti huo unaonesha mjamzito anayefanya mazoezi mara kwa mara hupunguza uwezekano wa kuongeza kupata kisukari, ugonjwa ambao huwatesa zaidi kinamama waliopo katika hali hiyo.
Hata hivyo, kwa wenye dalili za ugonjwa huo inapaswa kujihadhari zaidi, ikiwezekana kwa kuongeza muda wa mazoezi ili kuimarisha uwezekano wa mwili kukabiliana nao na maradhi mengine nyemelezi.

“mara nyingi wajawazito hufanyiwa upasuaji kutokana na watoto tumboni kuwa wakubwa au kukaa vibaya, hivyo kwa kufanya mazoezi tarajia mtoto atapungua na iwapo utakuwa na afya bora utajifungua bila ‘kisu’,” anasema mtafiti huyo.

Katika utafiti huo, inaelezwa mtoto anayezaliwa na mama mwenye mazoezi huwa mjanja zaidi kwa kuwa amezoweshwa tumboni ‘kuruka ruka na kutotulia’.  Hata wakati wa kujifungua, watoto wa namna hiyo hutoka haraka tumboni tofauti na wale wanaozaliwa na kinamama wasiofanya mazoezi.

Utaratibu unaotokana na hamasa ya kufanya mazoezi kwa wajawazito nchini Uingereza unachangia asilimia 25 ya vizazi visivyotokana na upasuaji sawa na zaidi ya watoto 190,000 kwa mwaka ambao ni sawa na idadi ya watoto wote waliokuwa wakizaliwa barani Ulaya miaka ya mwanzoni mwa 1980.

Kabla ya miaka ya 1990 hadi 2000 watoto waliokuwa wanazaliwa nchini humo kwa upasuaji, robo walipoteza maisha kutokana na kushambuliwa kwa urahisi na bacteria katika sehemu za vitovu na hawakuwa na mfumo imara wa ulinzi wa mwili.

Hata hivyo, theluthi ya idadi hiyo walikuwa wakiambulia maambukizi mbalimbali au ugonjwa wa kifua (asthema).

Dk Ruiz anasema hospitali hazipaswi kuwashauri tu wajawazito kuhusu mazoezi, bali zitenge nafasi kwa ajili ya kuwasimamia ili kuwasaidia kujifungua salama.

Daktari wa wanawake na watoto wa hospitali ya Mwananyamala jijini Dar Es Salaam, Dk Godfrey Chale anasema sababu za wajawazito kujifungua kwa upasuaji hutegemeana na tatizo analokuwa nalo mzazi.

“hapana, hakuna uhusiano sababu za uzazi wa upasuaji hutegemea na tatizo la mama kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua inaweza kutokea dharura,”  anasema.

Dk Chale anasema mazoezi kwa mjamzito yana faida na ni muhimu, isipokuwa mpaka apate ushauri wa kitabibu kabla hajayaanza.

“hata kwa asiyekuwa mjamzito, mazoezi ni muhimu, lakini ni lazima apate ushauri wa daktari kabla ya kuanza ili ushauri huo wa kitabibu uambatane na masharti iwapo mama atakuwa na tatizo la kiafya,” anasema.
Share:

No comments:

Post a Comment