Monday, November 21, 2016

MLO KAMILI UNAVYOPUNGUZA MAGONJWA, KUIMARISHA AFYA

mlo kamili unavyopunguza magonjwa

Takwimu za mwaka 2013 za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndiyo chanzo kikubwa cha vifo vya binadamu ulimwenguni.  Yanachangia kupoteza maisha ya binadamu kwa asilimia 63 ya vifo vyote kila mwaka.  Magonjwa haya huua watu zaidi ya milioni 36 kwa kipindi hicho.

Asilimia 80 ya vifo vinavyosababishwa na magonjwa haya hutokea nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania.  Makadirio yanaonesha ifikapo mwaka 2020, magonjwa haya yatasababisha vifo kwa asilimia 73 na ukubwa wake kuwa zaidi ya asilimia 60 ya magonjwa yote duniani.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza hayasambazwi kwa mtu mwingine kwa kuwa hakuna vimelea vyake mwilini vinavyohusiana nayo.  Magonjwa haya ni kama vile mshtuko wa moyo na mishipa ya damu, figo, saratani na kisukari.

Ripoti za kitaalamu nchini zinaonesha wananchi wengi wanaoishi miji mikubwa kama Dar Es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Tanga wanakabiliwa na magonjwa haya ambayo hayagunduliki kwa urahisi kwa sababu ya matumizi ya vyakula na vinywaji visivyozingatia mlo kamili.

Kuna watu duniani huugua mara chache sana.  Lakini wapo wengine ambao karibu nusu ya kipato chao cha kila mwezi au mwaka wanakitumia kwenye tiba ya miili yao.  Tofauti hii ya uimara wa afya unatokana na aina ya chakula cha kila mmoja na mfumo wa maisha.

Wananchi wanahitaji elimu juu ya kukabiliana na magonjwa haya kikamilifu.  Elimu hii inatakiwa ielekezwe kubadili mtindo na mfumo wa maisha, ikiwamo kula mlo kamili na kufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho.

Mlo kamili una sifa kuu mbili; mlo wenye virutubisho vyote muhimu vilivyo kwenye kiwango sahihi kwa mujibu wa mahitaji ya mwili.  Makundi mbalimbali yana mahitaji tofauti ya chakula.  Mfano, watoto na wazee mahitaji yao ya chakula ni tofauti.

Hakuna chakula kimoja chenye virutubisho vyote vinavyohitajika kwa mwili ili kuusaidia kufanya kazi vizuri na kupambana na maambukizi ya magonjwa ya aina mbalimbali.

Kwa hiyo, mlo kamili lazima uwe na vyakula kutoka makundi ya wanga, protini, mafuta, vitamin, madini, nyuzilishe na maji ya kunywa ili kila moja litoe virutubisho vinavyohitajika kujenga mwili na kuongeza uwezo wa kukabiliana na maradhi.

Kutokana na majukumu yanayowakabili watu siku hizi ni kawaida kuona wanakula huku wakitembea au kufanya kazi nyingine kama vile kusoma barua pepe, gazeti au kutumia simu ya mkononi.

Ulaji wa aina hii unaweza kudhuru siha zetu.  Mlo kamili ni silaha kubwa kwa uhai wa binadamu kwa sababu unaimarisha mwili na akili ya mhusika hivyo kuweza kufanikisha masuala mengi kutokana na uthabiti wa afya yake.

Mlo huu ni muhimu zaidi kwa watoto, wazee, wagonjwa, wajawazito na makundi yenye mahitaji maalumu kwa ajili ya afya njema kimwili na kiakili.  Husaidia kuwafanya wawe sehemu ya jamii hivyo kujumuika bila mipaka ya kiafya.

Vilevile, mlo kamili unaupa mwili kinga ya kupambana na maradhi, kudhibiti unene na uzito uliopitiliza, pia humuwezesha mtu kupata usingizi bila kutumia dawa.  Unene na kitambi ni matatizo makubwa katika maisha ya zama hizi.

Jambo lingine la kuzingatia ni kuwa mlo kamili lazima uendane na kufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho, na kupata muda wa kutosha wa kulala.  Inapendekezwa kulala walau saa tano mpaka nane kwa siku kwa mtu mzima.
Share:

No comments:

Post a Comment