Tuesday, February 21, 2017

LISHE BORA KWA MGONJWA WA UKIMWI




Ingawa vita dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) vinaendelea kushika kasi huku utafiti wa kuipata chanjo itakayoutokomeza ugonjwa huu ukiendelea kwenye mataifa mbalimbali duniani, wagonjwa wake wanahitaji matunzo makini.
Serikali imetangaza wote watakaogundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huu kuanza kutumia dawa za kupunguza makali (ARVs) mara moja.
Virusi vya Ukimwi vinapunguza uwezo wa mwili kufyonza chakula kutoka tumboni hivyo kuufanya mwili kuwa dhaifu kuhimili maambukizi ya magonjwa nyemelezi kama vile kuharisha sana na Kifua Kikuu (TB).
Hivyo basi, matumizi sahihi ya dawa za kufubaza na kupunguza makali ya virusi hivyo (ARVs) na lishe bora ni njia muhimu za kuimarisha afya ya mtu anayeishi na VVU.
Watu wanaoishi na VVU wanatakiwa kula vyakula kutoka mafungu yote ili wapate nishati, protini, mafuta, vitamin, madini, nyuzilishe na kunywa maji kwa kiasi cha kutosha mahitaji ya mwili.
Mwili wa mgonjwa wa ukimwi unahitaji nishati ya kutosha ili kukabili nguvu ya virusi vinavyosababisha maambukizi ya maradhi mengine pia.  Kwa hiyo, mlo wake lazima uwe na vyakula vya kumpa nishati kwa wingi kama vile ugali wa kila aina, wali, ndizi, mikate, chapati, mihogo na viazi.
Vyakula hivyo visikobolewe ili kuupa mwili nyuzilishe na virutubisho vingine na kumuepushia uwezekano wa kupata unene uliopitiliza na kisukari.
Wakati wa maandalizi ya vyakula vya mgonjwa, mafuta yawekwe kwa kiasi kidogo ili kuongezea ladha, kuupa mwili nishati na kuusaidia kufyonza vitamin A, D,E na K.
Watu wenye VVU wanatakiwa kutumia sukari, mafuta na chumvi kwa kiasi kidogo ili kuepusha magonjwa sugu kama kisukari, moyo na presha ya kupanda na uzito kupita kiasi.
Mtu anayeishi na VVU anatakiwa kupata mlo ambao una vyakula vyenye protini ili kuimarisha kinga za mwili.  Vyakula vyenye protini kwa wingi kama vile soya, maharage, jamii zote za karanga na njugu, mayai, maziwa, mtindi, samaki, kuku, ndege na nyama havitakiwi kukosekana.
Ili mfumo wa kinga wa mtu mwenye VVU ufanye kazi vizuri ni lazima mwili wake upate vitamin na madini ya kutosha.  Mwili unapata vitamin na madini kwa wingi kutoka kwenye matunda na mbogamboga pia zinaupa mwili nyuzilishe ambazo ni muhimu kwa kuzuia unene kupita kiasi na kansa ya utumbo.
Maji wanayokunywa watu wanaoishi na VVU lazima yawe safi na salama ili kuepusha maambukizi ya magonjwa ya kuharisha na homa ya matumbo.  Hata maji ya kutengenezea juisi au barafu yawe safi na salama pia.
Zaidi ya hayo, watu wenye VVU wale milo mitatu au zaidi kwa siku.  Vilevile wanywe juisi safi ya asili, maziwa ya moto, mtindi, maji ya dafu na supu ili kuongeza maji mwilini na kuufanya mwili kufanya kazi vizuri.
Watu hao wasinywe pombe wala kuvuta sigara au kutumia tumbaku ili kinga yao ya mwili isidhoofike zaidi na kuruhusu maambukizi kwa haraka.

Share:

No comments:

Post a Comment