Maambukizi ya njia ya mkojo au UTI ni tatizo linalowapata
watu wengi hasa wanawake na kujirudia mara kwa mara. Wanawake wamekuwa wakiugua bila kufahamu
namna ya kupunguza tatizo hili.
Zipo njia rahisi ambazo zikifanyika zinaweza kusaidia
kupunguza au kuzuia mwanamke kupata UTI mara kwa mara. Moja ya njia ya kujikinga na ugonjwa huu ni
kunywa maji mengi kila siku, kwa mtu mzima mwenye uzito kuanzia kilo 72, anywe
lita 1.5 mpaka mbili kwa siku.
Hii itamfanya apate haja ndogo mara kwa mara hivyo kutowaruhusu
bakteria kujenga makazi kwenye njia ya mkojo.
Inashauriwa kuepuka kuubana mkojo kwa muda mrefu, badala yake, hakikisha
unakwenda haja ndogo kila unapohisi kufanya hivyo.
Kwa wanawake walio kwenye siku zao, wanashauriwa kubadili
pedi mara mbili au mara tatu kwa siku. Kuvaa
taulo hizo za kike kwa muda mrefu hutoa nafasi kwa bakteria wanaosababisha UTI
kusababisha maradhi hayo.
Kwa wanawake wa rika lolote, haitakiwi kujisafisha ukeni kwa
sabuni zenye kemikali au kujipulizia marashi yoyote sehemu hizo hata kutumia
pedi zenye kemikali kukata harufu. Mambo
haya yanaharibu kinga ya maeneo hayo.
Unapojisafisha baada ya kujisaidia anzia mbele kurudi nyuma
kuepusha bakteria walio eneo la haja kubwa kuingia kwenye njia ya mkojo. Zingatia hili kila unapojichamba.
Usafi wa choo ni kitu kingine muhimu. Mwaga maji kabla ya kwenda haja na tumia maji
safi kujisafisha sehemu za siri baada ya kumaliza. Weka mazingira ya mwili wako safi ili kuepuka
maambukizi haya.
Kwa wenye wenza wanashauriwa kuepuka kujamiiana kinyume na
maumbile kwani chanzo cha ugonjwa huu ni bakteria walio kwenye njia ya haja
kubwa.
Safisha uke kabla ya kushiriki tendo la ndoa na nenda haja
ndogo baada ya kumaliza kujamiiana. Kama
kuna haja, tumia mipira yenye vilainishi au mafuta ili kupunguza michubuko
ukeni ambayo uwepo wake ni mazalia ya vimelea.
Kausha uke kwa kitambaa safi na kikavu, vaa nguo za ndani
zilizotengenezwa kwa pamba ili kutokana na uwezo wake wa kunyonya maji
kirahisi.
Vaa nguo za ndani zisizobana mwili na kuepuka zinazobana au
zilizotengezwa kwa nailoni au silki kwani hazinyonyi maji au jasho hivyo
kutengeneza mazingira ya mazalia ya vimelea wanaosababisha UTI.
Oga maji yanayotiririka kwani husaidia kuondoa uchafu na
vimelea kirahisi vilivyopo. Ikitakiwa kutumia
maji yaliyotulia, hakikisha unatumia chombo cha peke yako. Hii huwa ngumu kwa wanaoishi kwenye jamii
mfano wanafunzi lakini kwa kuzingatia afya, inabidi iwe hivyo.
Wajawazito wapo kweye hatari zaidi ya kupata maradhi haya
hivyo ni vizuri kwao na kula lishe bora na mlo uliosheheni protini, mboga za
majani na matunda ili kujenga kinga imara ya mwili. Hilo lifanyike sanjari na kuzingatia usafi.
Wajawazito wanatahadharishwa kutokurupuka kutumia dawa kwa
ajili ya kutibu UTI kwani si dawa zote ni salama kwao. Inapotakiwa kufanya hivyo basi iwe kwa ruhusa
ya daktari anayekutibu na kushauri dawa ambayo haitaathiri ujauzito ulionao.
Unapohisi dalili au viashiria vya awali,
unashauriwa kwenda hospitalini kwa ajili ya uchunguzi, matibabu na
ushauri. Epuka matibabu ya kienyeji
mtaani kutoka kwa watu wasio na sifa stahiki za kutoa matibabu ya
binadamu. Shikamana na matibabu ya
wataalamu wa afya na usikatishe dozi.
No comments:
Post a Comment