Mwili wa mwanadamu ni moja ya mashine kubwa na ngumu
kujifunza inavyofanya kazi, wanadamu tumeumbwa kuwa na hofu au wasiwasi kama
sehemu ya kujihami na matukio ya kila siku tunayokutana nayo.
Lakini hofu ina kiwango chake ambapo inapopitiliza inaweza
kuwa ni tatizo linalohitaji matibabu na ushauri.
Wataalam wa afya ya akili wanaitambua hofu au wasiwasi
uliokithiri kama Generalised Anxiety Disorder (GAD). Tatizo hili huwakosesha ajira baadhi ya watu
kutokana na kutojiamini katika usaili wa kazi au wanafunzi wanaofanya mitihani.
Hofu iliyopitiliza huambatana na wasiwasi kupita juu ya
maisha ya kila siku pamoja na matukio yake bila mhusika kuwa na sababu maalum
ya kuwa na hofu hiyo.
Watu wenye kuhisi hofu kubwa bila sababu yoyote ya msingi ya
kuwafanya wawe hivyo. Mara nyingi watu
wenye tatizo hili huhisi janga kubwa litawatokea karibuni au maafa yatawakumba
katika maisha yao na daima hawaachi kuwa na hofu juu ya familia zao, fedha,
afya, ajira, masomo, au biashara zao.
Maisha yao ya kila siku huwa na mchanganyiko wa hofu, wasiwasi
na huzuni, kiasi kwamba hatimaye hofu hutawala mawazo ya mhusika na kuingilia
ufanisi wake kazini, kwenye masomo, shughuli za kijamii au uhusiano na mwenza
wake.
Inakadiriwa watu wazima milioni nne mpaka tano nchini
Marekani hukumbwa na tatizo hili kila mwaka.
Hapa nchini hakuna takwimu zinaonesha ukubwa wa tatizo hili.
Kwa kawaida, wanawake huathiriwa zaidi kuliko wanaume. Aidha hofu iliyopitiliza mara nyingi huanza
kipindi cha utoto mara nyingi kabla ya ujana ingawa inaweza kutokea ukubwani.
Dalili
Hofu isiyo na kikomo huathiri uwezo wa mtu kufikiri ingawa
baadaye humletea matatizo ya kiafya. Hali
hii inaweza kuambatana na dalili mbalimbali siyo tu zinazohusu kufikiri na
akili bali utendaji kazi wa mwili.
Baadhi ya dalili hizo ni kuwa na hisia ya kuwepo kwa janga,
kwamba kitu kibaya kitatokea muda wowote na hatari inamnyemelea mhusika.
Hofu kuu, kujihisi kutaka kukimbia, kuondoka mbali na hatari
hiyo.
Rangi ya ngozi kuwa ‘nyeupe’ kama mtu aliyeishiwa damu au
kuhisi ngozi kuwaka moto na koo kubana.
Wengine huhisi kama koo limefunga au wamekabwa na kitu kooni,
kuchanganyikiwa, kuhisi kutengwa na ulimwengu, kupoteza hisia, kutojitambua
mwenyewe, kuhisi kizunguzungu na kichwa kuuma kuwa chepesi.
Wapo wanaopepesuka wanapotembea au kuwa mvurugo wa hisia,
hofu ya kurukwa akili na kupoteza uwezo wa kujidhibiti. Nyingine ni kuhisi kama vile kuna kitu
kinachobana kichwani (kama uliyezungushiwa Kamba au rubberband), kujihisi
baridi au joto kali ingawa hali ya hewa yaweza kuwa ya kawaida.
Dalili nyingine ni kushindwa kujituliza, kuhisi kitu
kinakaba tumboni, kichefuchefu, ganzi au kuchomachoma sehemu Fulani za mwili na
kuziba masikio na mapigo ya moyo kudunda kwa kasi.
Moyo kwenda kasi isivyo kawaida, maumivu makali kifuani,
shingoni, kwenye mabega, kichwani au usoni ni dalili nyingine za
kuzingatia. Kuhisi kukosa hewa au
kupumua kwa shida na kutokwa jasho.
Kubanwa kifua, kutetemeka iwe ndani kwa ndani au
kunakoonekana na watu wengine, kuchafuka tumbo, kuhisi haja ndogo au kubwa mara
kwa mara, kutapika, uchovu wa mara kwa mara, kupata usingizi kwa shida au
kulala usingizi wa mang’amung’amu.
Sababu
Chanzo halisi cha hofu kupita kiasi hakifahamiki. Hata hivyo kuna baadhi ya vitu ambavyo vimegundulika
kuwa vinachangia kuwepo kwa tatizo hili miongoni mwa watu.
Vitu au mambo hayo ni pamoja na vinasaba au genetics. Baadhi ya utafiti unaonesha vinasaba vina
nafasi kubwa ya kumfanya mtu wa familia yenye matatizo ya kuwa na hofu
iliyopitiliza naye kuwa na uwezekano mkubwa wa kuyapata. Hii inamaanisha, hofu iliyopitiliza inaweza
kurithiwa miongoni mwa wanafamilia.
Mfumo wa kemikali za ubongo ni sababu nyingine. Kuwepo kwa hofu iliyopitiliza kumehusishwa na
kuwapo kwa kiwango kisicho sahihi cha baadhi ya kemikali zinazosaidia
kusafirisha taarifa katika ubongo yaani neurotransmitters.
Kazi ya kemikali hizi ni kupitisha taarifa na ujumbe kutoka Seli
moja ya neva mpaka seli nyingine. Iwapo kemikali
hizi zitakuwa katika kiwango kisicho sahihi ama kupungua au kuongezeka, taarifa
hazitaweza kusafirishwa kama kawaida na kutoufikia ubongo. Hali hii inaweza kusababisha mabadiliko
katika utendaji kazi wa ubongo na hatimaye mhusika kupatwa na hofu
iliyopitiliza.
Mazingira. Inaelezwa,
matukio kama vile ajali, kuumia au matukio yenye msongo mkubwa kama vile
kunyanyaswa kwa namna yeyote ile, kufiwa na mtu unayempenda, talaka, kufukuzwa
kazi huweza kuwa chanzo cha hofu iliyopitiliza.
Wanafunzi wanaobadilisha au kufukuzwa shule wanaweza kuwa na
hofu iliyopitiliza. GAD huwa mbaya
mhusika anapokuwa na msongo wa mawazo. Aidha,
matumizi ya vilevi kama vile pombe, sigara hata kahawa yanaweza kuchangia tatizo
hili.
Waliowahi kuwa watumiaji wakubwa wa vitu hivyo kisha
wakaacha ghafla, wapo kwenye hatari ya kukumbwa na tatizo hili pia.
Vipimo na uchunguzi
Kabla ya kumfanyia uchunguzi wa mwili mzima kufahamu kama
hana tatizo jingine la mwili linaweza kumletea dalili za hofu iliyopitiliza,
daktari anapaswa kufahamu historia ya mgonjwa.
Iwapo daktari atabaini mgonjwa alikuwa akisumbuliwa na
dalili hizi kwa muda mwingi yaani miezi sita au Zaidi, ni Dhahiri ana GAD. Dalili hizi ni lazima ziingilie na kuathiri
maisha ya kila siku.
Pamoja na kuwa hakuna kipimo cha kuweza kugundua ugonjwa
huu, daktari pia anaweza kuagiza kufanyika kwa vipimo vingine ili kuchunguza
iwapo mgonjwa ana tatizo jingine lolote la kiafya.
Matibabu
Iwapo uchunguzi utaonesha mgonjwa hana tatizo jingine lolote
mwilini, daktari wa masuala ya afya ya akili atatakiwa kumhudumia. Matibabu yake kwa kawaida hujuisha dawa na
tiba ya kujitambua yaani cognitive-behavioral
therapy.
Hofu iliyopitiliza haina ya moja kwa moja. Hata hivyo kuna baadhi ya mambo ambayo
hutumika kupunguza makali yake. Mambo hayo
ni pamoja na kuacha au kupunguza matumizi ya baadhi ya vyakula au vinywaji kama
vile kahawa, chai, cola au chokleti.
Kufanya mazoezi mep[esi ya mwili ikiwamo
kutembea, kukimbia na kuogelea kila siku angalau kwa nusu saa na kutafuta
ushauri nasaha pindi unapoumizwa moyo au nafsi ni mambo yanayoshauriwa.
No comments:
Post a Comment