Ngozi ni muhimu kwa kila binadamu, hivyo kuhitaji kulindwa
ili isidhurike na kuuathiri mwili licha ya kuwapo kwa zaidi ya magonjwa 6,000
yanayoweza kuushambulia.
Yapo magonjwa ya ngozi ambayo yakimpata mtu hupona haraka na
kuiacha ikiwa katika hali yake ingawa mengine ni ya kudumu na yakitibiwa
huchukua muda mrefu kupona, hivyo kumkosesha raha mgonjwa.
Vitiligo au mbaraga ni moja ya magonjwa ya kudumu ya ngozi
ambayo huwanyima uhuru waathirika kutokana na kuhofia kutengwa na jamii, ingawa
wapo wachache walioikubali hali hiyo na kuishi kwa mafanikio.
Dk Zeinabbas Ladha anasema ugonjwa huu ni miongoni mwa
maradhi yanayotokea baada ya kinga za mwili kujishambulia (autoimmune reaction)
na kuathiri seli za melanocytes (melanini), zinazotengeza rangi ya ngozi na
kusababisha mabaka meupe katika baadhi ya maeneo ya mwili.
Kila mtu huzaliwa na chembechembe za melanini, hivyo ngozi
yake ama kuwa nyeupe au nyeusi na pindi zinaposhambuliwa ngozi hupoteza rangi
yake halisi na kupata maambukizi ya ugonjwa wa vitiligo.
Anasema ugonjwa huu unaweza kutokea sehemu yoyote ya mwili
na hausababishwi na bakteria wala vijidudu.
Wagonjwa wengi, anasema wanaathirika zaidi katika maeneo yanayopigwa na
jua kama vile usoni, mikononi, maeneo ya shingo na sehemu nyingine za mwili
ingawa unaweza ukajitokeza sehemu yoyote.
Kitabibu, ugonjwa huu hauhusiani na kitu chochote mwilini
isipokuwa kushambuliwa kwa chembechembe za melanini zinazotengeneza rangi ya
ngozi.
Anasema sababu nyingine ya kupata ugonjwa wa vitiligo ni
urithi kutoka miongoni mwa ndugu wa familia moja. Kwamba, mtu anayezaliwa kutoka kwenye familia
ambayo imewahi kuwa na mtu mwenye ugonjwa huu naye anaweza akaugua.
Dalili
Tofauti na ilivyo kwa maradhi mengine, mgonjwa wa vitiligo hapati
dalili zozote mfano maumivu, kuwashwa au homa bali huanza kuona mabaka meupe au
madoa yakijitokeza katika ngozi yake.
“ugonjwa huanza kwa sehemu ya ngozi kupoteza rangi yake
halisi na kuenea kwa mabaka meupe yanayoficha ngozi halisi,” anasema Dk Ladha.
Kwa baadhi ya watu, ugonjwa husambaa mwilini ingawa kuna
baadhi ambao huweza kuchukua muda mrefu kusambaa mwilini.
“ugonjwa huu hautabiriki, leo unaweza kuja na mabaka
machache lakini kesho ukasambaa. Unaweza
kuwa na baka upande mmoja lakini baada ya siku chache ukajikuta una mabaka
karibu mwili mzima,” anasema Dk Ladha.
Vitiligo hauchagui umri wala jinsia na mara nyingi huwapata
vijana ingawa uwezekano mkubwa ni kuwapata watu wenye umri kati ya miaka 20
mpaka 40. Kwa mtu mwenye chembechembe za
ugonjwa huu, mpaka anapofikisha miaka 40 tayari dalili zake zitakuwa
zimeshajitokeza.
Kuhusu tofauti ya maradhi haya na watu wenye ualbino,
anasema kuna uhusiano mdogo. “Watu wenye
ulemavu wa ngozi wanakosa kabisa chembechembe za melanini zinazoweza kuwapa
rangi ya ngozi wakati wenye vitiligo huwa na upungufu kwenye baadhi ya sehemu
za mwili,” anasema.
Athari
Anasema mara nyingi wagonjwa wa vitiligo wanaathirika
kisaikolojia kutokana na kubaguliwa na jamii inayowazunguka kwa hofu ya
kuambukizwa wakiamini kuwa nao jirani kunaongeza uwezekano huo.
Imani ya wengi itokanayo na kutofahamu ukweli wa vitiligo,
anasema ndiyo inayoongeza unyanyapaa kwenye jamii kwa kudhani ugonjwa huu una
chembechembe za ualbino, hivyo kutokana na imani za kishirikina.
Kutokana na vitiligo, mgonjwa ana uwezekano mkubwa wa kupata
saratani ya ngozi pindi akipigwa na mwanga wa jua hasa kwenye sehemu
zilizoathirika jambo ambalo wanatakiwa kuwa makini nalo wakati wote.
Matibabu
Kwa sasa, anasema, ugonjwa huu hauna tiba ya uhakika bali
zipo dawa za kupaka ili kuzuia kuendelea kusambaa kwake.
Dk Syriacus Buguzi anasema vitiligo ni kama saratani na njia
pekee ya kukabiliana nao ni kuiondoa sehemu iliyoathirika, vinginevyo
utaendelea kusambaa mwilini kadri mabadiliko kwenye seli husika yatakavyokuwa yakishamiri.
“Unaanzia kwenye kinga za mwili, hivyo hakuna namna ya
uhakika kuongeza uthabiti wa kinga hizo,” anasema Dk Syriacus.
Pamoja na hayo yote, kuna njia ambazo mgonjwa wa vitiligo
anashauriwa kuzitumia ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea ambazo
zinahiusisha kujifunika sehemu alizoathirika zisipigwe na mwanga wa jua, kupaka
dawa ya kuzuia mwanga wa jua kuharibu ngozi na utumiaji wa taa za ultraviolet
light ambazo husaidia kufubaza madoa yaliyotokea.
Kwa watoto wa kike, utumiaji wa vipodozi husaidia kuficha
maeneo yaliyoathirika na kuzuia ngozi isiendelee kudhurika.
Duniani
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Vitiligo ya
Kimataifa (VR Foundation), zinaonesha zaidi ya watu milioni 65 ni waathirika wa
ugonjwa huu duniani kote.
Mara nyingi wagonjwa wa vitiligo wamekuwa wanakata tamaa na
wakati mwingine wakijifungia ndani, kufadhaika na msongo.
Mrembo na mwanamitindo wa kimataifa wa Canada, Challente
Brown almaarufu kama Winnie Harlow, baada ya kuyatia masikio yake pamba na
kutojali kinachosemwa na wanaomtazama amefanikiwa kutimiza ndoto zake licha ya
kuwa na maradhi haya.
Lee Thomas, mtangazi wa Fox 2, kituo cha runinga nchini
Marekani hulazimika kupaka vipodozi usoni ili kuweka mlinganiko wa ngozi yake
hasa maeneo yanayozunguka macho, pua na masikio yaliyoathirika na vitiligo ili
kuepuka kuonekana akiwa na rangi mbili mbele ya kamera za kituo hicho.
Mwanamuziki mkongwe duniani na mfalme wa pop, marehemu
Michael Jackson amewahi kusemwa kuwa na maradhi haya mikononi na kadri miaka ilivyozidi
kwenda ulikuwa ukisambaa mwilini mwake.
Jamii
Theresia Maganga (60) mkazi wa mtoni kijichi jijini Dar Es
Salaam ambaye ni mgonjwa wa vitiligo akiwa na mabaka chini ya shingo, anasema
alishangaa baada ya kuona hali hiyo inamtokea.
Anasema amekuwa akiulizwa maswali mengi kutoka kwa watu
ambao kila mmoja akiongea lake juu ya ugonjwa huo na baadhi wakikaa nae mbali,
wakidhani unaambukiza jambo ambalo linamnyima uhuru wa kuchangamana nao.
“Nalazimika kuvaa nguo zinazoficha eneo hili ili watu
wasinishangae,” anasema Theresia.
Anasema alitumia gharama kubwa kutafuta dawa za kumsaidia
kupona kabla hajafahamu kuwa hauna tiba, lakini bado hali iliendelea kuwa
vilevile huku hofu ya kuathirika ikizidi kumjaa baada ya kuona dalili za madoa
miguuni.
No comments:
Post a Comment