Ingawa hakuna umri maalamu ambao mwanamke anaweza kushika
ujauzito baada ya kukidhi vigezo vya kibaiolojia, tunafahamu kwamba kuanzia
miaka 35 uwezo huo hupungua na changamoto za uzazi huongezeka.
Japokuwa hilo sio lazima litokee kwa watu wote kwani wapo
wanawake ambao hupata ujauzito wakiwa na miaka 40 na 50 bila tatizo lolote,
ushauri wa daktari au mkunga ni muhimu kwa watu wa umri huo.
Kutokana na mfumo wa elimu na matakwa ya kitaaluma, wanawake
wengi huchelewa kuzaa miaka hii licha ya ukweli kwamba uzazi kwao una mipaka
inayozingatia umri na uwezo wa mwili kutimiza matakwa hayo.
Japokuwa haimaanishi tatizo la kiafya kwa mwanamke anayeamua
kuzaa baada ya umri huo, kuna masuala kadhaa ya kuzingatia ili kupunguza
changamoto zinazoweza kujitokeza.
Kila mwanamke anayo idadi maalamu ya mayai ambayo huzaliwa
nayo. Mayai haya hupungua kadri umri
unavyoenda. Kuanzia miaka 30 na 40,
idadi na ubora wa mayai haya hupungua. Kupungua
kwa ubora wa mayai yako kunaongeza ugumu wa kupata ujauzito kwa wakati ingawa
si wakati wote.
Ukiacha haya, zipo changamoto ambazo mwanamke anayetaka
kushika ujauzito baada ya miaka 35 anapaswa kuzizingatia na kufuata ushauri wa
daktari au mkunga atakayemuwezesha kukabiliana nazo.
Pacha
Uwezekano wa kuzaa pacha huongezeka kadri umri
unavyosogea. Uzoefu unaonesha, mjamzito
wa zaidi ya miaka 35 yupo kwenye uwezekano wa kuzaa pacha watatu.
Kwa wale wanaotumia dawa za kutafuta mimba uwezekano huo
huongezeka Zaidi. Kuwa na ujauzito wa
aina hii kwa umri huo huambatana na changamoto kadhaa zinazophitaji uangalizi
wa daktari ili kuepuka kujifunza kabla ya wakati, kifafa cha mimba na kisukari
cha mimba.
Magonjwa
Uwezekano wa kuugua kisukari cha mimba huongezeka kwa
wajawazito wa umri huo. Ili kukabiliana
na changamoto zinazoweza kujitokeza, mjamzito atapaswa kuzingatia masharti ya
chakula ili kutozidisha kiasi cha sukari kwenye damu yake.
Hii inaweza kuhitaji matibabu endapo hali itakuwa
mbaya. Hatua za maksudi zisipochukuliwa
kutibu kisukari hiki kitaathiri ukuaji wa mtoto au watoto watakaozaliwa na
maisha yake hapo baadae.
Shinikizo la damu kwa wajawazito wa umri huu ni kawaida
pia. Uangalizi wa daktari na matibabu
ni muhimu kwao vilevile.
Njiti
Upo uwezekano wa kujifungua kabla ya muda hivyo mtoto au
watoto wakawa njiti na wenye uzito mdogo.
Kwa kawaida, mtoto aliyezaliwa kabla ya majuma 37 ya ujauzito, kitabibu,
huwa njiti. Watoto hawa huwa na
changamoto kadhaa ambazo zinahitaji umakini kuwatunza mpaka wakue.
Upasuaji
Upasuaji ni suala jingine ambalo mjamzito wa umri mkubwa
anashauriwa kama njia ya kujifungua. Kadri
umri unavyoenda ndivyo matatizo ya kujifungua kwa njia ya kawaida
yanavyoongezeka.
Matatizo ya mara kwa mara ni kujiviringa kwa kitovu cha mtoto
jambo linalohatarisha maisha yake hivyo huhitaji upasuaji.
Matatizo ya Kuzaliwa
Nayo
Ingawa ni nadra, wanawake katika umri huo wapo kwenye hatari
ya kujifungua watoto wenye matatizo ya chembembuzi au chromosomal abnormalities ambayo husababisha ugonjwa uitwao down syndrome (DS).
Inaelezwa, DS hutokea kwa mtoto mmoja kati ya vizazi 700,
mara nyingi kwa wanawake wenye umri mkubwa ingawa hata walio chini ya miaka
huweza kujifungua.
Watoto hawa pia wanaelezwa, kuwa na uwezekano wa kuzaliwa na
matatizo ya moyo. Tatizo jingine ambalo
linaweza kujitokeza ni kuharibika kwa mimba.
Wanawake wa umri huo, wana hatari ya mimba zao kuharibika.
Licha ya changamoto hizi zilizoelezwa bado zipo namna za
kuweza kuishi na ujauzito na kujifungua salama.
Kujali afya kwenye kipindi chote cha ujauzito kwa ajili ya afya ya mama
na mtoto ni muhimu bila kujali umri.
Mimba Salama
Kabla ya kupata ujauzito, wanawake wenye umri huu
wanashauriwa kupata maelekezo ya daktari na kufahamu mambo muhimu wanayotakiwa
kuyazingatia. Ushauri kuhusu namna ya
kurahisisha kushika mimba, lishe kwa kipindi hicho na historia na maradhi ni
muhimu kwa wanawake hawa.
Kuhudhuria kliniki ni muhimu kwa wajawazito wote ila zaidi kwa
wenye umri huo. Wajawazito hawa
wanapaswa kuzingatia hili kwa ajili ya afya zao na watoto wanaotarajia
kujifungua.
Lishe bora ni suala jingine muhimu. Wakati wa ujauzito, wanawake wanahitaji vitamin
D, folic acid, calcium na virutubisho
vingine. Wanashauriwa kunywa maji mengi
na kula mlo kamili wenye matunda na mboga za majani kwa wingi.
Ingawa huwa kunakuwa na uchovu, kufanya mazoezi ya viungo ni
muhimu. Haya husaidia kufungua njia ya
uzazi na kupunguza uwezekano wa kufanyiwa upasuaji.
Mazoezi pia husaidia kuimarisha afya ya mwili mzima. Kila program mpya ya mazoezi unayoifanya ni
lazima iruhusiwe na daktari wako anayekuchunguza katika kipindi hiki kabla
hujaianza.
Achana na vitu vinavyohatarisha afya. Unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara pamoja
na dawa za kusisimua mwili ni miongoni mwa mengi usiyoshauriwa kuyafanya wakati
huu. Hata utumiaji wa baadhi ya dawa kwa
ajili ya maradhi yoyote uliyonayo yanapaswa kuwa na kibali cha daktari.
Vipimo vya jumla. Ili
kupunguza uwezekano wa mtoto kuzaliwa na matatizo, daktari anaweza akashauri vipimo
kadhaa ili kujiridhisha. Vipo vipimo
vingi kama vile; damu, mpangilio na ubora wa seli au DNA.
Inashauriwa, unapotaka kushika ujauzito kwenye
umri huo, ni vyema kufahamu hatari zilizopo na kuchukua tahadhari za kiafya kwa
ajili yako na mtoto.
No comments:
Post a Comment