Ni kawaida watoto wadogo kunyonya kidole kutokana na
mahitaji ya kimwili na kisaikolojia.
Mtoto huanza kunyonya kidole endapo hapati maziwa ya kutosha. Mara nyingine husababishwa na matatizo ya
kihisia.
Kwa mtoto, kunyonya kidole ni namna ya kujifariji. Mtoto asipotosheka kila anaponyonya huanza
kunyonya kidole ambako humfanya apunguze njaa.
Kisaikolojia; hujibembeleza na kujisikia salama.
Mara nyingi mtoto ataacha kunyonya kidole akiwa na umri kati
ya miaka mitatu mpaka sita, ingawa wengine huendelea hadi ukubwani.
Inasemekana kuwa tabia hii huanzia tumboni baada ya wiki
kumi na tatu za ujauzito na huendelea mpaka mtoto anapozaliwa ingawa wazazi
wengi hugundua hilo mtoto anapofikisha umri wa miezi miwili mpaka mitatu.
Zipo faida zilizothibitika za watoto kunyonya kidole. Nyingine zinaendelea kuchunguzwa. Baadhi ya watafiti wanadai unyonyaji huo
huimarisha kinga ya mwili. Watafiti hao
wanadai unyonyaji wa dole gumba na ung’ataji wa kucha husaidia kuzuia mzio au
allergy.
Hasara
Kama ilivyo kwa masuala mengine yoyote, hili nalo linalo
hasara zake. Zipo zitokanazo na mtazamo
na imani za jamii husika na zile za kimuonekano.
Kwenye jamii zilizopo, baadhi ya watu huamini mtoto
anayenyonya kidole anajipunguzia uwezo wa kuzingatia masomo, hivyo kuwa mjinga
jambo ambalo halijathibitika.
Upo uwezekano wa mdomo hasa kuathirika. Inaelezwa kuwa ‘lips’ zinaweza kulegea
kutokana na uzito wa kidole sambamba na mtoto kuchelewa kuwa na ufahamu
kutokana hutumia muda mwingi kunyonya kidole.
Wazazi wanashauriwa kuwa macho ili kunusuru hali hii.
Endapo mtoto ataendelea kunyonya hata akiwa na umri mkubwa
kidogo inaweza kusababisha meno kutojipanga vizuri kwenye fizi. Madaktari wa kinywa wamehusisha mpangilio
mbaya wa meno na kunyonya kidole hasa gumba, kwani meno husukumwa kwenda mbele
au kujipanga vibaya na hivyo kuathiri muonekano wa mhusika.
Daktari bingwa wa meno, Christopher Ruhinda wa Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH) anathibitisha hili.
“Ni kweli. Nguvu (presha)
anayotumia mtoto kunyonya kidole inaharibu mpangilio wa meno. Mara nyingi yanatoka nje na mdomo hushindwa
kufunga,” anasema Dk Ruhinda.
Kunyonya kidole sio hatari ikiwa mtoto ataacha kabla ya miaka
mitano. Kama mtoto atashindwa kuacha
kunyonya kidole mpaka baada ya umri huo kuna uwezekano wa meno yake kutojipanga
vizuri na kuota yakiwa yamebebana au kuwa na meno yasiyokutana.
Watoto wanaonyonya kidole baada ya miaka minne au mitano wana
hatari ya kupata tatizo hili hivyo kuathiri muonekano wao wa sura na hata
matatizo ya kuongea vizuri. Hii huweza
kutokea kutokana na kulegea kwa lips ambazo ni muhimu kwa matamshi ya baadhi ya
maneno. Meno yaliyokosa nafasi au yenye
nafasi kubwa nayo yana athari kwenye matamshi.
Kutokana na kunyonya huko mtoto atapata tatizo la matamshi na viungo vya
mdomo mfano ulimi kutoka nje wakati wa kuongea.
Inategemea na ukubwa wa athari. Kama mpangilio haujawa mkubwa sana mpangilio
mbaya huweza kujirekebisha wenyewe iwapo mtoto ataacha kunyonya kidole. Kwa wale wanaopitiliza wanahitaji huduma za
mtaalamu wa meno (orthodontist) kufanya marekebisho.
Ipo mifano kadhaa ya watu waliowahi kufanya upasuaji wa fizi
ili kurekebisha mpangilio wa meno kuupata muonekano wanaouhitaji.
Cha kufanya
Inashauriwa kutomkataza mtoto kunyonya kidole akiwa chini ya
miaka minne au mitano isipokuwa kama kuna tatizo linalojitokeza au mtoto
akianza ghafla kufanya, hivyo baada ya miezi kumi tangu azaliwe na ikiambatana
na kuvuta nywele.
Ili kupunguza uwezekano huo, mama anayenyonyesha anapaswa
kula vyakula vyenye lishe kamili vitakavyosaidia mwili kutengeneza maziwa ya
kutosha kumnyonyesha na kumshibisha mtoto kila wakati, hivyo kumuepusha
kunyonya kidole.
Kwa mtoto anayenyonya, wazazi au walezi wanapaswa kumueleza
kwa upole wakitumia lugha laini ikibidi kumuahidi zawadi nzuri ili akubali
kuacha kunyonya kidole.
Kumuanzisha shule ni njia nyingine inayoweza kumsaidia mtoto
kuacha kunyonya kidole. Shule kutamfanya
aone aibu hasa atakapokuwa anataniwa na wenzake anaosoma na kucheza nao.
Njia mbadala pia zinaweza zikatumika. Hizi zitamsaidia kuacha mapema zaidi. Kupaka pilipili vidole vyake ili akinyonya
awashwe na ukali wa atakaokutana nao itamfanya asirudie tena kufanya hivyo
ingawa kutakuwa na jukumu la kubembeleza atakapokuwa analia baada ya kunyonya
kidole.
Kushiriki michezo inayoshughulisha mikono kwa muda mwingi ni
njia nyingine ya kufanikisha suala hili.
Unaweza ukampa midoli au wanasesere, au acheze na wenzake ili mradi
viganja vyake viwe na shughuli ya kufanya na kumnyima nafasi ya kunyonya
kidole.
Pia, unaweza kumnunulia nyonyo za plastiki ili umpe anyonye
badala ya kidole. Hii itamfanya asipate
muda wa kuzoea kunyonya kidole na hatotumia muda mwingi kunyonya nyonyo hizo.
Wengine kuwavalisha watoto mipira ya mikono au viganja (gloves)
na kuwafanya washindwe kunyonya vidole.
Iwapo vyote vitashindikana basi mzazi au mlezi asisite
kuwaona madaktari wa afya ya meno na kinywa kwa msaada zaidi.
No comments:
Post a Comment