Wanawake wote huwa na dalili tofauti kipindi cha ujauzito,
ukiacha zile za jumla. Wapo wanaohisi
kichefuchefu wakati wengine hutapika na baadhi wakishindwa kula baadhi ya
vyakula.
Kadri ujauzito unavyoendelea kukua, mjamzito hushauriwa
kuhudhuria kliniki ili kufuatilia maendeleo ya kiumbe kilichomo tumboni. Hii husaidia kufanikisha uzazi salama kwa
afya ya mama na mtoto mtarajiwa.
Jambo lililozoeleka ni wajawazito wengi kuhudhuria na kupata vipimo vya jumla, wachache huwa
wanafuatilia hali za meno na kinywa.
Tahadhali ni kwamba ujauzito unaweza kusababisha matatizo ya afya meno
na kinywa cha mama husika.
Kutokana na uwezekano huo, ni muhimu kumuona daktari wa
kinywa na meno wakati wa ujauzito kwa ajili ya uchunguzi, ushauri au tiba pale
itakapohitajika ndani ya muda huo.
Ni muhimu kuzingatia upigaji wa mswaki kwa kutumia dawa ya
meno yenye madini na floridi mara mbili kwa siku na kufanya flosi mara moja kwa
siku. Kutunza usafi wa kinywa chako
huweza kusaidia afya ya mama na mtoto.
Kipindi cha ujauzito
Kuwa mjamzito kunaambatana na majukumu mengi ambayo
humuandama mama bila kujali ni ujauzito wake wa ngapi. Pamoja na hayo yote, utunzaji wa afya ya
kinywa ni jukumu ambalo halikwepeki.
Ni vizuri kuzungumza na daktari wa kinywa na meno kuhusu
namna nzuri ya kukitunza ili kutoathiri afya yako kwa muda wote wa ujauzito
pamoja na kuchagua dawa nzuri za kutumia kufanya hivyo kila
itakapohitajika. Kupiga mswaki kwa dawa
ya meno yenye madini ya floridi mara mbili kwa siku na kufanya flosi ni
utaratibu ambao hautakiwi kuachwa. Kama
kutahitajika kubadili dawa kutokana na mabadiliko hayo, ifanyike hivyo lakini
mfumo huo wa usafi uendelee kama inavyopendekezwa.
Muone daktari
Kwa wanawake wengi, kwenda kumuona daktari wa meno kisha
kupata matibabu wakati wa ujauzito ni jambo salama. Kitu muhimu kinachohitajika ni kutosahau
kumueleza umri wa ujauzito husika.
Licha ya umri wa ujauzito, daktari atahitaji kufahamu dawa
za meno unazotumia kila siku na matibabu ya magonjwa mengine yoyote unayotibiwa
ili ajue namna nzuri ya kukuhudumia bila kumuathiri mtoto.
Mabadiliko ya kinywa
Wakati wa ujauzito baadhi ya wanawake huweza kupata ugonjwa
wa kuvimba au fizi kutoa damu hivyo kuwa nyekundu na kuuma pia. Unaweza kuzuia ugonjwa huu kwa kuhakikisha
meno na kinywa vinakuwa safi kwa kipindi chote cha ujauzito.
Daktari wa kinywa na meno anaweza kupendekeza kufanya usafi
mara nyingi zaidi ya mbili kwa siku zinazofanywa na watu wote ili kuidhibiti
hali hii. Unapoona mabadiliko yoyote
mwilini wakati wa ujauzito, tafadhali muone daktari wa meno, hii ni kwa sababu
hali hii isipotibiwa inaweza kuleta madhara zaidi.
Vyakula
Je, unajua kwamba meno ya mtoto wako aliye tumboni huanza
kutengenezwa kuanzia mwezi wa tatu mpaka wa sita wa ujauzito? Hii ndiyo maana
unahitaji virutubisho vya kutosha hasa Vitamini A, C na D, protini, pamoja na
madini ya kalsiumu na fosforasi.
Wakati ni jambo la kawaida kwa mama mjamzito kupenda kula
zaidi, kula vyakula vya sukari inaweza kuwa ni kukaribisha kuoza kwa meno. Unapokula tafadhali tumia zaidi vyakula
vyenye kiasi kidogo cha sukari na ambavyo vina virutubisho vyote muhimu kwa
faida yako na mtoto aliye tumboni.
Vyakula kama vile matunda, mboga za majani na jibini ni
muhimu na itakuwa vizuri kufuata ushauri wa daktari kuhusu aina ya vyakula
unavyopaswa kutumia kipindi hiki.
No comments:
Post a Comment