Tuesday, May 30, 2017

UNAWEZA KUNYWA MAZIWA MBADALA YATOKANAYO NA MIMEA

maziwa ya soya

Kwa muda mrefu maziwa ya ng’ombe na mifugo mingine yamekuwa maarufu nchini na kwingineko duniani.

Lakini maendeleo ya teknolojia na kuongezeka kwa mahitaji, kumeongeza ubunifu.

Ongezeko la watu na tofauti za kiafya kumesababisha mahitaji ya maziwa kuwa tofauti.  Watu wanaokula chakula kwa mpangilio maalumu kutokana na ushauri wa daktari (diet) au wenye mzio hawawezi kutumia maziwa haya.  Hata watoto na wagonjwa hushauriwa kunywa aina fulani za maziwa.

Kutokana na mahitaji hayo, wataalam wa tiba lishe wamefanikisha utengenezaji wa maziwa kutokana na mazao ya shambani.  Licha ya wanyama, watu sasa wanaweza kunywa maziwa yatokanayo na soya, mchele au, lozi ama badama (almond).

Hata hivyo, kila maziwa yanaelezwa kuwa na faida na hasara zake kwa afya ya binadamu kutokana na uthabiti wa afya, mahitaji ya kiafya na upendeleo wa mhusika.  Kwa mfano; watoto walioacha kunyonya, wenye zaidi ya miaka mitano na wajawazito wanahitaji zaidi protini, Vitamin D na madini ya calcium.  Virutubisho hivi hupatikana zaidi kwenye maziwa ya mifugo.

Kwa upande mwingine, watu wanaopunguza uzito kutokana na magonjwa ya moyo au uzito uliopitiliza wanatakiwa kuyaepuka maziwa hayo kwa sababu yana kiwango kikubwa cha virutubisho vinavyoongeza uzito na lehemu.

Maziwa ya Ng’ombe

Maziwa haya yana faida nyingi na hupatikana kirahisi madukani.  Yana virutubisho vingi vya protini, vitamin, calcium na madini ambayo ambayo ni muhimu kwa watoto na wazee.

Tahadhali inatolewa kwa watu wenye mafuta mengi mwilini kwani maziwa haya huchochea ongezeko hilo hivyo kuweza kuongeza hatari kwa wenye matatizo ya moyo au wanaotaka kupunguza uzito.  Yanaelezwa kusababisha uzio kwa watoto na watu wazima pia.

Maziwa ya Mchele

Maziwa haya hutengenezwa kutokana na mchanganyiko wa maji na mchele.  Yanaelezwa kuwa ndiyo ya mwisho kwa kusababisha mzio kwa watumiaji wa umri wowote hivyo kuwafaa zaidi watu wenye matatizo hayo.

Ingawa yanaweza kusindikwa na kuongezewa calcium na vitamin D, maziwa haya yanaelezwa kwamba sio chanzo halisi cha virutubisho hivyo.

Hali ni hiyo kwa maziwa ya soya au lozi

Licha ya kutosababisha mzio, faida nyingine za maziwa ya mchele zinaelezwa kuwa ni chanzo kizuri cha madini ya calcium.  Vilevile, yanashauriwa kutumiwa na watu waliozuiliwa kula nyama na bidhaa zake.

Maziwa haya inabainishwa kuwa yana kiasi kikubwa cha wanga na kidogo cha protini, hivyo kutokuwa chaguo zuri kwa wagonjwa wa kisukari na wote wanaohitaji zaidi protini kama vile wanariadha na wazee.

Maziwa ya Soya

Yanatengenezwa kutokana na soya.  Nayo ni chaguo kwa wasioshauriwa kula nyama na bidhaa zake.  Hayana lehemu wala mafuta kwa sababu yanatokana na mimea ingawa ni chanzo kizuri cha protini na madini ya calcium endapo yatasindikwa.

Yanaelezwa kuwa chanzo kizuri cha protini, vitamin A, B12 na D, na madini ya potassium.  Protini yake inalinganishwa na iliyomo kwenye maziwa ya ng’ombe.

Yana kiasi kidogo cha mafuta hivyo kuwafaa zaidi wenye magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu.

Tahadhali ni kwa watu wenye matatizo ya matezi.  Matumizi makubwa ya soya yanaelezwa kusababisha maambukizi ya matezi.  Utafiti uliofanywa chuo kikuu cha Havard kilichopo nchini Marekani mwaka 2008 ulionesha matumizi hayo hupunguza nguvu za kiume.

Maziwa ya Lozi (almond)

Maziwa haya hutengenezwa kutokana na lozi au badama kama zinavyoitwa kwenye baadhi ya maeneo.  Yanaelezwa kuwa na calories chache zaidi kuliko maziwa ya aina nyingine yoyote.

Hayana lehemu wala mafuta.  Ingawa lozi zenyewe ni chanzo kizuri cha protini maziwa yake hayana sifa hii.  Siyo chanzo kizuri cha madini ya calcium ingawa mengi yanayouzwa huongezwa madini haya pamoja na vitamin D.  Ni chanzo cha uhakika cha vitamini A pia.

Hasara zake ni kwamba sio chanzo kizuri cha protini kama yalivyo maziwa mengine labda ikiongezwa.  Hayana calcium pia ambayo ni muhimu kwa watu wenye udhaifu wa mifupa hasa wanawake waliofunga hedhi.

Watu wenye mzio na lozi au jamii za karanga wanashauriwa kuyaepuka maziwa haya.  Yana virutubisho vya carrageenan ambavyo husababisha matatizo kwenye mfumo wa usagaji chakula.
Share:

No comments:

Post a Comment