Nikiwa mmoja wa waunga mkono katika juhudi za kukabiliana na
magonjwa yasiyoambukiza yaani non-communicable disease leo nitawapa dondoo
zinazohusu mazoezi mepesi.
Kama ilivyoendelea kuelezwa na serikali kuwa kutakuwa na
utaratibu wa kufanya mazoezi kila Jumamosi ya pili ya mwisho wa mwezi. Ninafahamu wengi wanaweza kujitokeza lakini
je wanajua ni kwa muda gani wafanye mazoezi yawe ya aina gani.
Ieleweke kuwa mazoezi yanayotakiwa kufanywa ni mazoezi
mepesi kitaalamu hujulikana kama aerobic exercise.
Mazoezi mepesi ni pamoja na kukimbia mbio za taratibu,
kutembea, kuogelea, kuruka Kamba, kufanya kazi ndogo ndogo, kuendesha baiskeli
na kucheza mziki.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zimebaini kuwa mazoezi
mepesi ndiyo yanayochangia watu kuishi maisha marefu zaidi. Hii ni hutokana na mazoezi haya kumuepusha
mtu na magonjwa ya moyo, kisukari, shinikizo la damu na unene uliopitiliza.
Mazoezi haya kama yakifanywa kwa ufanisi ndiyo silaha bora
ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo kisukari, magonjwa ya moyo na
unene uliopitiliza.
Mazoezi mepesi hayahitaji kwenda katika vituo vya mazoezi
vya kulipia, yanafanyika katika maeneo ya wazi na njia za watembea kwa miguu.
Faida ya mazoezi haya ni pamoja na kuchoma mafuta
yaliyorundikana, kuimarisha afya ya moyo na mapafu hivyo kukufanya kuwa na
upumuaji mzuri na mzunguko imara wa damu.
Vilevile hukusaidia kukupa mwili mkakamavu na utulivu wa
kiakili na kimwili.
Mazoezi haya yanakufanya kuepukana na msongo wa mawazo
ambalo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza.
Wataalam wa sayansi ya michezo wanashauri mazoezi mepesi
yafanyike angalau mara tano kwa wiki, kwa siku iwe kwa dakika 30-40.
Muda huu ndiyo unakubalika na wanasayansi wa michezo kuwa
unaufanya mwili kutumia mafuta yaliyorundikana.
Kama ni kutembea umbali unaopendekezwa kitaalam ni kilomita
2 kwa siku. Mazoezi mepesi yana ufanisi zaidi
kama yakifanywa nyakati za jioni au asubuhi.
Pale unapofanya mazoezi kila mara na kwa muda mrefu ndivyo
pia mwili unatumia zaidi mafuta yaliyorundikana hivyo kuwezesha kudhibiti
unene/uzito mkubwa.
Hivyo kuanzishwa kwa utaratibu wa kufanya mazoezi kila
Jumamosi ya pili ya mwezi na Serikali ichukuliwe kuwa ni kichochezi cha
kutufanya kupenda kufanya mazoezi mepesi.
Isije ikatokea kuwa unafanya tu mazoezi hayo katika siku
hiyo tu ilyoelekezwa, utakuwa unajidanganya kwani ili kuweza kupata afya njema
inahitajika kujenga tabia ya kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara kwa muda
mrefu.
No comments:
Post a Comment