Kadri umri unavyozidi kusogea, ni kawaida kwa wengi wetu
kupoteza uwezo wa kusikia. Upotevu huu
wa uwezo wa kusikia kutokana na umri, kitabibu, hutambulika kama presbycusis.
Watu kati ya 100 wenye zaidi ya miaka 65 kwa kiasi fulani,
hupoteza uwezo wao wa kusikia. Kwa wenye
zaidi ya miaka 70; mtu mmoja kati ya wawili ana tatizo la kusikia.
Sababu za hali kuwakumba watu wa kundi hilo ni umri mkubwa,
mazingira yenye kelele na uwapo wa kiasi kikubwa cha nta kwenye masikio.
Kiwango kikubwa cha nta inayotengenezwa katika mrija mdogo
uliopo sikioni ambao huelekeza sauti kwenye ngoma ya sikio, ikiondolewa kwa
kiasi kinachohitajika, usikivu hurejea na kuwa wa kawaida.
Dalili
Zipo dalili ambazo hujitokeza kwa mtu aliye kwenye hatari ya
kupoteza uwezo wa kusikia vizuri. Kupata
tabu kidogo wakati wa kufuatilia maongezi yanayotolewa kwa sauti ambayo awali
ulikuwa unaweza kuisikia na kuelewa kinachozungumzwa ni miongoni mwake.
Kupata shida kusikia herufi za konsonanti na mara kadhaa
kuwaambia watu wangeze sauti wakati wanaongea nawe ni dalili nyingine. Wapo wanaoongeza sauti ya radio au runinga
ili waweze kusikia vizuri.
Kutopenda kuchangia kwenye maongezi ya zaidi ya mtu mmoja
kutokana na kushindwa kufuatilia kinachojadiliwa na kukwepa kwenda maeneo
ambayo kuna sauti nyingi kwa wakati mmoja.
Sababu
Kuna sababu nyingi zinazochangia kutokea kwa mushkeri huu
kwa wazee ambazo zinajumuisha tatizo ndani ya sikio. Umri mkubwa na kuishi kwenye eneo lenye
kelele kwa muda mrefu vinaweza kuharibu au kuua chembe hai maalumu za fahamu
zilizopo ndani ya sikio zinazoitwa ‘cochlea.’
Cochlea hubadili sauti iliyo kwenye mfumo wa mitetemo kuwa
kwenye mfumo wa umeme maalumu unaoweza kusafirishwa na mfumo wa fahamu kwenda
kwenye ubongo kwa ajili ya kutafsiriwa.
Chembehai hizo za fahamu zinapokuwa zimeharibika au kufa
huwa hakuna uwezekano wa sauti kufika kwenye ubongo kwa ajili ya tafsiri, hivyo
mhusika kushindwa kutambua au kutofautisha sauti. Aina hii ya upotevu wa kusikia hutambulika
kama sensorineural hearing loss na ukitokea huwa ni vigumu kurudi kwenye hali
ya kawaida ya usikivu.
Sababu nyingine ni maradhi au kukua kwa mishipa ya
sikio. Maradhi tofauti ya sikio, pamoja
na ukuaji usio wa kawaida wa mfupa wa fuvu unaozunguka sikio la nje na la kati
yanaweza kusababisha upotevu wa kusikia.
Hii hutokana na maradhi au mfupa huo kuingilia utendaji wa
kawaida wa sikio kwa kuingilia usafirishaji wa mawimbi ya sauti kutoka sikioni
kwenda ubongoni kwa ajili ya tafsiri.
Inaweza kusababishwa kutoboka kwa ngoma ya sikio. Ngoma ya sikio au tympanic membrane kama
inavyoitwa kitabibu, huweza kutoboka kutokana na msukumo mkubwa wa mawimbi
yanayosababishwa na sauti kubwa kupita kiasi au kubadilika ghafla kwa msukumo
wan je wa hewa. Uingizaji wa vitu vyenye
ncha sikioni nayo huweza kutoboa ngoma ya sikio pamoja na maambukizi ya baadhi
ya maradhi.
Walio hatarini
Kutokana na kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi pamoja na
kugawanyika kwa chembehai maalumu za fahamu zilizo ndani ya cochlea, watu wenye
umri mkubwa wapo kwenye hatari hii.
Wanaoishi kwenye mazingira yenye kelele muda mrefu wapo
kwenye uwezekano wa kuharibu chembehai maalumu za fahamu zinazotumika kusikia
kutokana na mitetemo ya sauti kubwa kwa muda mrefu hivyo chembehai hizo
kuharibika na kushindwa kufanya kazi.
Kuharibika kwa chembehai hizi hupunguza ubora wa mawimbi ya
sauti kwenda kwenye ubongo kwa ajili ya
kufanyiwa tafsiri na mhusika kupata maana ya kinachozungumzwa na kumfikia.
Wanaopokea sauti kubwa za ghafla kama mlipuko wa bomu, mlio
wa risasi au kufungua redio kwa sauti kubwa ghafla huweza kusababisha ngoma ya
sikio kutoboka.
Kingine kinachoweza kutokea ni kuharibika kwa chembehai
maalum zilizo ndani ya eneo la ndani la sikio hivyo kushindwa kusafirisha sauti
kwenda kwenye ubongo kwa ajili ya tafsiri.
Mazingira ya kazi hasa yale yenye sauti kubwa huweza
kusababisha upotevu wa moja kwa moja wa kusikia. Hii hutokana na uharibifu unaotokea kwenye
chembehai maalum za usikivu zilizoko kwenye cochlea.
Wanaotumia dawa ambazo husababisha madhara kwenye sikio kwa
muda mrfu zikiwamo za kuua vimelea vya maradhi huwa na madhara yasiyotakiwa
kwenye masikio na uwezo wa kusikia.
Madhara haya huwa ni yamuda mfupi tu lakini kwa watu
wanaozitumia dawa hizo kwa muda mrrefu huweza kupata madhara ya kudumu kwa
kupoteza uwezo wao wa kusikia.
Wenye maradhi yanayotokana na maambukizi ya vimelea huweza
kupata madhara kwenye masikio na kuhatarisha uwezo wao wa kusikia.
Matibabu
Matibabu hutolewa kwa kukabiliana na chanzo cha tatizo kwa
kuzingatia uwezekano wa tatizo husika kupona ama kutopona. Kwa ambao tatizo lao linaweza kupona matibabu
yake hulenga kukabiliana na chanzo cha tatizo.
Matibabu hayo yanaweza kuhusisha kuondoa nta masikioni kwa
ambao tatizo la usikivu limetokana na kiasi kikubwa cha nta kwenye mfereji
unaounganisha sikio la nje na lile la kati.
Hawa tiba yao ni kutolewa kwa nta iliyozidi.
Waliopata majeraha kutokana na maradhi au ajali hufanyiwa
upasuaji ili kuondoa au kukausha maji au usaha kwenye eneo la kati au la ndani
la sikio. Endapo kukausha kutashindikana
mrija maalum ambao utafanya kazi ya kuondoa maji hayo na kuruhusu hali ya
kawaida ya utendaji kazi wa sikio kurejea unaweza ukawekwa.
Kwa ambao tatizo linatokana na madhara yaliyotokea eneo la
ndani la sikio huweza kusaidiwa kwa kuwekewa vifaa maalum ambavyo hukuza sauti
kiasi cha kutosha kusababisha chembehai chache za fahamu kuisafirisha sauti
hiyo kuipeleka kwenye ubongo kwa ajili ya tafsiri.
Baadhi huhitaji cochlea ya bandia. Hawa ni wale wenye tatizo ambalo haliwezi
kutibiwa na kurudisha uwezo unaotakiwa hivyo mhusika anaweza kufanyiwa
operesheni yenye lengo la kuweka cochlea nyingine ambayo ina uwezo wa kufanya
kazi.
Kinga na namna ya
kuishi
Ili kukabiliana na tatizo hili na kuishi salama, mtu mwenye
nalo wanatakiwa kumtazama anayeongea naye ili kufuatilia kinywa cha
anayezungumza. Hii husaidia kuelewa kitu
kinachoongelewa kwa kufuatia mwendo wa kinywa wa anayeongea.
Unaweza pia kuhakikisha sauti unayotaka kuisikia ndiyo sauti
pekee iliyopo kwenye eneo hilo kwa kuzuia sauti nyingine tofauti na hiyo
zisisikike (kwa mfano kama unaongea na mtu huku redio inawaka unaweza kuzima
redio ili uweze kile tu mwenzio anachozungumza).
Ikiwezekana, unaweza kumuomba mtu unayeongea naye aongeze
sauti na asiongee kwa kasi ili uweze kusikia vizuri na kukielewa kile
anachozungumza.
Unaweza pia chagua maeneo yasiyo na kelele kuyatumia kufanya
mazungumzo na wale unaotaka kuwasiliana nao.
Mgonjwa anashauriwa kujiepusha na maeneo yenye sauti kubwa
au kelele na kama anafanya kazi kwenye maeneo ya namna hiyo basi ahakikishe
anafunika masikio yake kwa kuvaa vizuizi vya sauti.
Unaposikiliza redio kwa kutumia spika za
masikioni au earphones hakikisha unafanya hivyo ukiwa umeweka sauti ya chini.
No comments:
Post a Comment