Watafiti nchini Japan wamegundua jinsi seli za mfumo wa
fahamu zinafaa kupandikizwa kwenye kongosho ili kutibu kisukari. Hii ni habari nzuri yenye kutia matumaini kwa
jamii ya wataalam wa tiba katika kukabiliana na ugonjwa wa kisukari
unaoambatana na madhara mbalimbali kama shinikizo la juu la damu, kiharusi,
kuharibika kwa figo na uoni hafifu au upofu.
Ripoti ya utafiti ambayo imechapishwa kwenye jarida la kitafiti la Embo
Molecular Medicine na mtandao wa Medical News Today inaonesha seli zinazovunwa
kutoka katika mfumo wa fahamu zinaweza kupandikizwa katika tezi la kongosho na
kumaliza tatizo la ukosefu wa seli za beta ambazo huhitajika kwa ajili ya
uzalishaji wa insulin. Kisukari ni
ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa kichocheo insulin kinachozalishwa na tezi
kongosho au la mtu anaweza kuwa na uwezo wa kuzalisha kichochezi hiki, lakini
kukapata ukinzani wa kutumiwa na seli za mwili.
Kuna aina kuu mbili za kisukari; cha aina ya kwanza na ya
pili, ingawa kipo pia kinachojitokeza wakati wa ujauzito.
Ikumbukwe kuwa katika aina ya kwanza kinga za mwili
inaziharibu seli zinazotengeza kichocheo cha insulin ambacho ndicho hutoa
maelekezo ya seli kutumia sukari kama chanzo cha nishati.
Wakati ikiwa hivyo, kisukari aina ya pili hutokea pale
kongosho linapoendelea kutengeza insulin kama kawaida, lakini hutokea ukinzani wa kuitumia mwilini kwa ajili ya kuzalisha nishati.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani za mwaka 2015 zinakadiria
watu zaidi ya 415 wanaishi wakiwa na maambukizi ya ugonjwa huu, idadi hii
inatarajiwa kufikia milioni 642 ifikapo mwaka 2040.
Mpaka sasa hakuna tiba yoyote ya ugonjwa huu, hali
inayowafanywa wagonjwa wa kisukari kutegemea zaidi kudhibiti kiwango cha sukari
mwilini ili kupunguza madhara yake.
Utafiti huo ulioongozwa na Dk Tomoko Kuwabara kutoka taasisi ya Utafiti
wa Afya ya Tsukuba (AIST) ya nchini Japan, ulilenga kuchunguza jinsi seli za
binadamu zinavyokua na kujigawa kulingana na kazi mbalimbali za mwili na
uwezekano wa kuzitumia seli mbalimbali kutekeleza majukumu tofauti na kawaida
yake.
Katika ufafanuzi wake, Dk Kuwabara anasema kwa vile kisukari
ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa aina moja ya seli, ugonjwa huu unaweza
kutibika kwa kutumia upandikizaji wa seli mpya zitakazotumika kuzalisha kichocheo
cha insulin.
Anasema, hata hivyo kwa vile kupandikiza seli za beta kutoka
seli kongosho za watu wengine ni ngumu kutokana na ukosefu wa watoaji, njia
muafaka ni kutumia seli za mfumo wa fahamu wa mgonjwa mwenyewe kufanikisha
upandikizaji huo.
Seli za mfumo wa fahamu zinazoweza kupandikizwa kwenye tezi
kongosho kwa urahisi zaidi ni zile zilizopo kwenye ubongo wa mbele zijulikanazo
kitaalamu kama hippocampus na olfactory bulb.
Kwa kawaida, seli za mfumo wa fahamu huzalisha kiwango
kidogo sana cha insulin tofauti na seli za tezi kongosho, hata hivyo, mara tu
baada ya kupandikizwa kwenye tezi kongosho, seli hizo zilianza kutoa kiwango
kiwango kikubwa cha kichocheo cha insulin na kiwango cha sukari katika damu
kilionekana kupungua kwa kiwango kikubwa.
“Na, hata seli zilizopandikizwa zilipoondolewa, kiwango cha
insulin kilishuka na kusababisha kupanda tena kwa kiwango cha sukari katika
damu.” Anasema Dk Kubawara.
Utafiti ulitumika kwa kutumia panya walioambukizwa ugonjwa
wa kisukari kisha upandikizaji wa majaribio ukafanywa kwa seli za mfumo wa
fahamu kwenda kwenye tezi kongosho.
Kwenye matokeo hayo yaliyoleta matumaini mapya, siyo tu
yalionesha uwezo wa seli za mfumo wa fahamu kudhibiti uzalishaji wa kichocheo
cha insulin, bali ukweli kuwa seli zinazohitajika kwa ajili ya upandikizaji
zinaweza kutoka kwa mgonjwa mwenyewe bila kuhitaji uwepo wa mtoaji (donor).
Akihitimisha, Dk Kubawara alisema matokeo ya utafiti wao
yameonesha uwezo mkubwa wa seli za mfumo wa fahamu kutibu kisukari bila
kuhitaji mabadiliko ya kinasaba au mtoaji (donor), hali ambayo inaleta
matumaini ya kuondokana na tatizo la ukosefu wa watoaji wa seli za upandikizaji
siku za mbele.
Dk Absolom Maiseri wa Hospitali ya Lugalo na Kituo cha Afya
Mgulani, anaunga mkono utafiti huu na kueleza kuwa wagonjwa wa aina ya kwanza
ya kisukari wanaweza kunufaika zaidi na matokeo haya.
Mara baada ya kugundulika, anasema wagonjwa hawa hutegemea
sindano ya kichochezi cha insulin zinazochomwa chini ya ngozi kwa maisha yao
yote. “Ugunduzi huu utapunguza maumivu
kwa wagonjwa pamoja na fedha nyingi wanazotumia kununua dawa hizi,” anasema.
Mtaalam wa maabara, Abdulraab Hassani ameupokea utafiti huu
lakini, anasema bado kunahitajika utafiti mwingine kuthibitisha kama
upandikizaji huu unaweza kuwa mbadala wa sindano ya insulin.
Ni vizuri jamii kuamka, moja ya njia rahisi za
kujikinga isiyo na gharama ni kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara au
kuushughulisha mwili kwa kazi tofauti zinazoufanya viungo vingi kutumika kwa
wakati mmoja.
No comments:
Post a Comment