Ulaji wa vyakula vibichi kama vile karanga, mihogo, nazi na
vinapoandaliwa kama kachumbali au saladi ni maarufu katika nchi yetu.
Mboga za majani ambazo hazijakomaa na bado mbichi ni chanzo
kizuri cha vitamin na madini ya aina mbalimbali. Washauri wa lishe wanahimiza ulaji wa kachumbali
na vyakula vingine vibichi.
Mboga kama matango, kabichi, vitunguu, nyanya na karoti ni
maarufu kwa utengenezaji wa kachumbali hapa nchini na kwingineko duniani. Pia, vyakula hivyo vikiwa na maganda yake
vitumike kutengeneza juisi ili kupata madini na vitamin kwa wingi.
Ulaji mbogamboga unaondoa tindikali inayozalishwa wakati
vyakula vingine vikisagwa tumboni kama vile nyama na jibini (cheese). Mboga za majani za kijani ni chanzo kikubwa
cha carotene inayobadilishwa mwilini na kuwa vitamin A. Mboga ni chanzo kizuri cha vitamin C pia.
Vitamin A ina kazi kubwa ya kuimarisha macho ili yaone
vizuri hasa wakati wa kiza.
Pia, inasaidia ukuaji na ufanyaji kazi wa chembehai na
kuimarisha kinga ya mwili. Vitamin C ina
kazi nyingi ikiwamo kuimarisha ufanyaji kazi wa chembehai, inaimarisha kinga,
inaponya mafua na vidonda. Baadhi ya
mboga zina protini au wanga.
Maharage na kunde ni chanzo kikubwa cha madini ya chuma na protini. Viazi mviringo na vitamu ni
chanzo kikubwa cha wanga.
Ingawa kupika vyakula kuna faida nyingi kama kuua vijidudu
vya maradhi na kukifanya kuwa rahisi kutafunwa na kusagwa tumboni, ni ukweli wa
miaka mingi kuwa kupika kunaharibu baadhi ya virutubisho vinavyopatikana katika
vyakula hivyo.
Vitamin na madini ni rahisi kuharibika na kupotea vikikutana
na moto.
Kwa upande mwingine, watu hawafahamu kuwa ulaji wa vyakula
vibichi ambavyo havikuoshwa vizuri ni chanzo cha magonjwa ya kuambukiza kama
homa ya matumbo, kipindupindu, tumbo la kuhara, kuhara damu, amiba na minyoo.
Kwa hiyo, lazima watu waoshe vizuri mbogamboga kwa kutumia
maji safi na salama ili kuondoa vijidudu vinavyoweza kusababisha maradhi.
Kuziosha vizuri kunaondoa dawa zilizotumika zikiwa shambani
pia.
Dawa hizi huwa ni sumu zinapoingia katika tumbo la binadamu
au wanyama.
Zaidi ya hayo, watu wawe makini kujua mahali
zilipozalishwa mbogamboga wanazozinunua kabla ya kuzitumia ili kujua aina ya
maandalizi wanayopaswa kuyafanya.
Miaka michache iliyopita, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam
kiliwahi kufanya utafiti kuhusu ubora wa mboga zinazozalishwa kando ya barabara
na zile zinazozalishwa katika bonde la mto Msimbazi, Jijini Dar Es Salaam.
Watafiti hawa walibaini kuwa baadhi ya mbogamboga hazifai
kuliwa na binadamu wala wanyama kutokana na kuwa na kemikali zinazodhuru afya.
Vilevile, mamlaka zinazohusika zikiwamo halmashauri na
manispaa mbalimbali nchini zichukue hatua kuzuwia kilimo cha mboga kando ya
barabara na karibu na vyanzo vya maji vyenye kemikali zinazoweza kudhuru afya
za walaji.
Sambamba na hayo, Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) ishirikishe na vyuo vikuu, taasisi za utafiti na wadau wengine ili kujua
ubora wa vyakula vinavyoliwa vikiwa vibichi.
No comments:
Post a Comment