Macho ni kiungo pekee mwilini kinachokuwezesha kuitambua
dunia na vilivyomo. Kuongezeka kwa
mahitaji ya binadamu kunakosababishwa na kukua kwa uchumi kunaongeza muda ambao
macho yanakuwa kazini.
Taka zinazotokana na uchafuzi wa mazingira, muda mrefu wa
kufanya kazi kwenye kompyuta na matumizi yaliyokithiri ya simu za mkononi
huchukua muda mwingi wa macho kuendelea kutumikishwa. Licha ya haya yote, bado watu wengi hawali
vyakula muhimu kwa afya ya macho yao.
Ama hawafahamu au hawajui kuwa chakula hasa virutubisho vilivyomo ni
muhimu kwa ajili ya kulinda uwezo wa macho kuona hata kwa wenye umri mkubwa.
Kitu muhimu ambacho wataalam wa masuala ya macho
wanapendekeza ni kutambua ukweli kwamba uwezo wetu wa kuona hutegemea aina ya
vyakula tunavyotumia kila siku.
Kanuni
Upo ushauri rahisi ambao wataalam wa macho wanashauri kila
mmoja kuuzingatia. Uchunguzi wa macho wa
mara kwa mara hata kama hakuna dalili hatarishi zilizojitokeza.
Wataalam wanasema vipimo hivi vinaweza kusaidia kugundua
tatizo ambalo dalili zake hazijaanza kujitokeza na kupendekeza matibabu
yatakayozuia madhara yake. Maradhi haya
yanaweza kuwa presha ya macho au glaucoma ama matatizo ya lensi ya jicho au
cataracts.
Wanashauri kufanya vipimo vya macho kila baada ya miaka
miwili ingawa daktari wako anaweza kupendekeza vinginevyo.
Macular degeneration; maradhi ya kupoteza uwezo wa kuona kadiri
umri unavyozidi kusogea ni tatizo linalowakabili watu wengi ulimwenguni lakini
yakibainika mapema mgonjwa anaweza kuishi vyema.
Kwa wanaopenda masuala ya urembo hasa wa macho, wanashauriwa
kuepuka vipodozi vilivyokwisha muda wake kwani vinaweza kusababisha maambukizi
na kuleta madhara makubwa kwa mhusika.
Vyakula
Ulaji wenye mpangilio una manufaa kwa ufanisi wa macho yako,
kinachotakiwa ni mchanganyiko makini wa vyakula muhimu kwenye mlo wako.
Mlo wenye matunda mengi na mboga za majani vinahitajika
zaidi kwa ajili ya afya ya macho yako. Umuhimu
wake huonekana zaidi virutubisho hivi vinapoimarisha kinga za mwili na
kupambana na seli zilizokufa (free radicals).
Mboga za majani hasa zenye kijani kibichi ndizo
zinazoshauriwa zaidi kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa uendelevu wa macho
kuona. Spinachi, matembele au kisamvu ni
baadhi ya mboga hizo.
Wataalam wanashauri kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta
mengi au sukari nyingi ingawa mafuta mazuri yanashauriwa. Yanayopendekezwa ni yale ya samaki…hakikisha
unakula mafuta mengi ya samaki kila wiki, ukiweza.
Licha ya mafuta ya samaki, ya karanga na mazao mengine ya
jamii ya njugu pia yanapendekezwa kwa ajili hiyo. Matunda hasa maparachichi ni chanzo kingine
cha virutubisho muhimu vya uimara wa macho.
Kubadili mfumo wa maisha hasa kwa kuepuka au kupunguza
uvutaji wa sigara na bidhaa nyingine za tumbaku kunashauriwa ili kukinga hatari
zinazoweza kujitokeza. Inashauriwa
kuepuka mionzi ya UV (Ultraviolet rays).
Madini na Virutubisho
Inashauriwa kuhakikisha kwenye kila mlo kunakuwa na
antioksidanti (antioxidants) hasa lutein na zeaxathin kutokana na umuhimu wake
wa kulilinda jicho kupoteza uwezo kwa sababu ya umri mkubwa (macula) au
hitilafu za lensi ya jicho (cataracts).
Lipo tatizo kubwa la kuwa na macho makavu hasa miongoni mwa wanawake
ambao kipindi chao cha hedhi kimekoma.
Mafuta ya samaki wa baharini ni suluhisho la tatizo hili. Yana wingi wa virutubisho vya omega 7 ambavyo
husaidia kurudisha vilainishi vya macho, yakiwamo machozi.
Kupata virutubisho hivi, unashauriwa kutumia
zaidi mafuta ya samaki endapo yatakosekana basi siyo mbaya ukitumia aside za
fati (fatty
acids) zinazouzwa kwenye maduka ya dawa.
No comments:
Post a Comment