Figo ni kiungo muhimu kwa ajili ya kuchuja vitu mbalimbali
ikiwamo sumu kwenye damu, mkojo na maji yasiyohitajika ili kuwa na kiwango
kinachohitajika cha maji na madini (electrolytes) mwilini.
Licha ya hayo, hufyonza madini na kemikali muhimu
kuzirudisha katika mzunguko wa damu huku ikitoa nje uchafu usiohitajika.
Kutokana na umuhimu wake, inashauriwa kuchukua hatua zote
makini ili kuepusha maambukizi yanayoweza kuathiri uwezo wa kiungo hiki
kufanyakazi kama inavyotakiwa. Magonjwa
mengi yanayoweza kuathiri figo husababishwa na mfumo wa maisha kama vile
unywaji wa pombe na uvutaji sigara.
Mfumo wa maisha ambao husababisha magonjwa yasiyoambukiza
kama vile kisukari yanaongeza hatari ya magonjwa ya figo au kama unavyotambulika
Chronic Kidney Disease (CKD).
Kushambuliwa kwa figo kunaweza kusababisha ikashindwa kabisa
kuendelea kufanyakazi, inapofikia katika hatua hii tiba sahihi huwa ni dialysis
au kuchuja maji yasiyohitajika mwilini na uchafu unaambatana na maji hayo.
Tiba hii hutolewa kwa wale ambao aidha figo zao zimeshindwa
kufanya kazi au wana upungufu wa figo moja ambayo huelemewa. Upo uwezekano wa mgonjwa kupandikizwa figo
nyingine kutoka kwa mchangiaji.
Matibabu haya yote hugharimu muda, fedha na rasilimali nyingine
za mgonjwa hivyo kuna umuhimu wa kujiepusha na mazingira hatarishi kwa kadri
inavyowezekana.
Miongoni mwa mambo muhimu ambayo yanashauriwa ni kuepuka
magonjwa yasiyoambukiza ambayo athari zake zina uwezekano mkubwa wa kufika
kwenye kiungo hiki na kukipotezea uelekeo wake.
Yapo magonjwa ambayo unapaswa kuyaepuka.
Kisukari
Kisukari ni moja ya magonjwa yanayoongoza kuleta athari
kwenye figo kwa kuharibu mirija inayopeleka damu, na inayofyonza damu kutoka
kwenye figo na kusababisha ishindwe kusafisha damu kwa usahihi.
Matokeo ya changamoto ni mwili kuwa na kiasi kikubwa cha
maji na chumvi kuliko inavyohitajika, hivyo kusababisha kuwapo kwa taka nyingi
mwilini.
Madhara mengine ni mkojo kushindwa kwenda kwenye kibofu,
kutokana na kuharibika mrija unaousafirisha kutoka kwenye figo kwenda kwenye
kibofu au urethra.
Kutokana na hili mkojo hulazimika kurudi kwenye figo na kuziweka kwenye hatari kutokana na msukumo mkubwa
unaokuwapo, wakati mwingine kutokea maambukizi ya njia ya mkojo.
Shinikizo la Juu la
Damu
Shinikizo la damu ni ugonjwa unaotokana na kuwapo kwa
msukumo mkubwa wa damu kuliko kawaida.
Ongezeko la msukumo huu kwenye mishipa ya damu husababishwa na mapigo ya
moyo kwenda kupita kiasi.
Msukumo wa damu mwilini unapokuwa mkubwa sana, unaweza
kusababisha mishipa ya damu hasa iliyopo kwenye figo kukaza, kuitengenezea
majeraha madogo na kutokana na msuguano unaotokana na msukumo mkubwa wa damu
uliopita; kuidhoofisha na kukosa nguvu.
Kutokana na hali hii basi, mishipa ya damu iliyopo kwenye
figo inaweza kuisababisha ishindwe kuchuja uchafu kama inavyotakiwa. Pia, vimiminika vinavyosalia ndani ya mishipa
ya damu baada ya figo kushindwa kufanya kazi kwa usahihi, vinaweza kuongeza
shinikizo la juu la damu na hatari zake.
Kukabiliana na shinikizo inashauriwa kula vyakula ambavyo
havina kiwango kikubwa cha mafuta, kufanya mazoezi ya viungo na kuzuia msongo
wa mawazo.
Lehemu
Lehemu au cholesterol ikizidi mwilini huleta shida. Kuzidi kwa mafuta haya kunatokana na ulaji wa
vyakula vyenye mafuta mengi hasa ya wanyama na kutofanya mazoezi.
Lehemu ikizidi mwilini, inaenda kujijenga ndani ya mishipa
ya damu ambayo inasafirisha damu kutoka na kuingia kwenye figo hivyo kuathiri
utendaji kazi wake.
Uwepo huu wa lehemu katika mishipa ya damu inaweza pia
ikasababisha shinikizo la juu la damu na kisukari. Vipimo vya damu vinaweza kuonesha kama
kiwango chako cha lehemu kipo juu ama la.
Matatizo wakati wa
haja ndogo (urine blockage)
Kama unashindwa kupata haja ndogo au unaipata kwa shida
inaweza kumaanisha mkojo unarudi kwenye figo kabla ya kufika kwenye kibofu na
inaweza kuleta madhara kwenye kibofu.
Kutokana na uwapo wa mkojo ambao unashindwa kutoka nje
unaongeza uwezekano wa kupata maambukizi kwenye figo na sehemu nyingine za
mwili. Tezi dume lililoongezeka ukubwa,
saratani ya tezi dume, uwepo wa mawe katika figo, saratani ya kibofu, damu
kuganda katika njia ya mkojo na saratani ya utumbo ni baadhi ya magonjwa
yanayosababisha tatizo hili.
Ni vyema kumuona daktari haraka au kama unaona mchanganyiko
wa damu unapokojoa.
Lupus
Mwili una mfumo kinga maalumu wa kujilinda na kujikinga
dhidi ya magonjwa mbalimbali kuingia mwilini kwa kutumia kinga zake
unaojulikana pia kama immune system ukiwa na jukumu la kushambulia viini vyote
vya magonjwa vinavyoingia mwilini.
Wakati mwingine mfumo huu hukosea na kushambulia tishu
mbalimbali za mwili na kusababisha ugonjwa wa lupus. Dalili zake viungo vya mwili kuuma, homa za
mara kwa mara, maumivu ya kifua, kunyonyoka kwa nywele, vidonda vya mdomo na
kuhisi kuchoka mara kwa mara.
Kinga za mwili zinaposhambulia tishu za mwili huweza kufika
mpaka kwenye figo na kusaabisha ugonjwa unaoitwa lupus nephritis ambao
huchangia kutokea kwa michubuko kwenye mirija inafyonza maji kutoka mwilini
hatimaye kuzifanya figo kushindwa kufanya kazi ipasavyo.
Mazoezi ya mara kwa mara na kufanya vipimo vya kitaalamu ni
mambo yanayoshauriwa kwa watu wote na muda wote. Hii ni bila kujali umri wa mhusika.
No comments:
Post a Comment