Friday, January 5, 2018

IELEWE SARATANI YA SHINGO YA UZAZI


Wadau na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya afya kote duniani huutumia mwezi huu kutathmini jitihada za kupambana na saratani ya shingo ya uzazi, ugonjwa unaoongoza kuua wanawake wengi kuliko aina nyingine yoyote ya saratani.

Hapo awali, wanawake walikuwa wanapoteza maisha baada ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu tofauti na hali ilivyo sasa kwani idadi ya wanawake wanaopoteza maisha kutokana na saratani hiyo imepungua kutokana na kampeni zilizofanyika kuongeza uelewa.

Wanawake hivi sasa hawana sababu ya kuendelea kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huu ingawa bado wanaendelea kufa.  Saratani ya shingo ya kizazi bado inaendelea kutishia maisha ya wanawake nchini.  Ripoti za karibuni zilizotolewa na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC) zinaarifu kuwepo kwa maelfu ya wanawake walio hatarini kupatikana na saratani ya kizazi katika miaka michache ijayo huku sababu kubwa ikiwa ni kukosa taarifa na uelewa wa kutosha.

Saratani ya shingo ya kizazi ni ugonjwa ambao huanzia na kukua kwenye mlango wa uzazi maarufu kama cervix ambayo ni sehemu nyembamba yenye uwazi inayoanzia ukeni hadi kwenye mfuko wa uzazi.

Saratani ya mfuko wa kizazi ndiyo inayoongoza kuua wanawake wengi kuliko aina nyingine ya saratani ingawa ikigundulika mapema kunakuwa na uwezekano mkubwa wa mgonjwa kupona.

Aidha, saratani ya shingo ya kizazi imethibitika kuwa ni saratani inayozuilika kirahisi kuliko nyingine zote.  Njia pekee ya kuzuia na kujikinga na saratani hii ni kupata chanjo ya HPV; Human Pappiloma Viruses ambayo ni aina ya virusi vinavyosababisha saratani hii.

Saratani hii huwashambulia wanawake pekee hivyo kumaanisha hatari ya kwanza ni mwanamke mwenyewe.  Mara nyingi hutokea katika umri wa kati.  Zaidi ya nusu ya wanawake wanaopimwa na kukutwa na saratani hii huwa na umri kuanzia miaka 30 hadi 60 ingawa huwapata pia wenye wastani wa miaka 20, mara chache.
Inakadiriwa, asilimia 20 ya wanawake kuanzia miaka 60 na kuendelea.

Sababu nyingine zinazomuweka mwanamke hatarini kupata ugonjwa huu ni uvutaji wa sigara na aina yoyote ya tumbaku, maambukizi ya ukimwi au magonjwa mengine ya ngono na hasa yanayojirudia, uzito uliopitiliza, umasikini na sababu za kurithi zinazotokana na historia ya ugonjwa kwenye familia.

Mwanamke wakati wote anashauriwa kuwa makini na dalili kuu za ugonjwa huu kwani kupitia hizo zitampa msukumo wa kuwahi hospitali kuwaona wahudumu wa afya na kupata vipimo ili kuiwahi saratani hii ikiwa kwenye hatua za awali.

Dalili kuu za saratani ya shingo ya kizazi ambazo mwanamke hapaswi kuzifumbia macho ni pamoja na kutokwa na damu kusikoendana na ratiba ya mzunguko wake wa hedhi, kutokwa na damu wakati au baada ya tendo la ndoa au wakati wa kujisafisha na hedhi isiyokoma kwa mwanamke ambaye hawezi kushika mimba kutokana na umri.

Dalili nyingine ni ya mara kwa mara maumivu chini ya kitovu, kutokwa na uchafu wenye rangi ya maziwa au njano unaoambatana na harufu mbaya na maumivu wakati wa haja ndogo.
Share:

No comments:

Post a Comment