Kwa kawaida, meno hutakiwa kuwa meupe lakini kutokana na
sababu mbalimbali huweza kuwa na rangi nyingine.
Meno yaliyoharibika rangi humuathiri mhusika
kisaikolojia. Kwa mfano anaweza
kujishtukia wakati anazungumza. Hali hii
husababisha kutojiamini anapokuwa na watu wenye meno meupe walau kuliko yeye
katika shughuli mbalimbali.
Kwa kuwa rangi ya meno itokanayo na kuzidi kwa madini ya
floridi huwa haitoki kwa kupiga mswaki, wengi wa waathirika hudhani meno yao ni
machafu hata baada ya kupiga mswaki.
Hali hii ni matokeo ya tatizo linalotokea kwenye tabaka la
nje la meno wakati wa utengenezwaji wa meno husika linalosababishwa na kuwapo
kwa kiasi kikubwa cha madini ya floridi kuliko kiwango kinachohitajika.
Hali hii husababisha tabaka la nje la jino lililoathirika
kuwa na madini mengine kwa kiwango kidogo wakati madini ya floridi yakiwa mengi
kupita kiasi huku tabaka hilo likiwa na vitundu vidogo vidogo (porosity). Hivyo kuyafanya yasiweze kusafishika kwa
kupiga mswaki.
Ukubwa wa tatizo hili kwa mhusika hutegemea vitu vingi kama
vile umri ambao muathirika amekumbwa na madini hayo kwa wingi au namna mwili
wake unavyoyapokea madini hayo. Sababu
nyingine ni ukuaji wa mifupa, hali ya lishe kwa ujumla na matatizo ya figo.
Wakati tatizo la kuzidi kwa madini ya floridi huathiri
mifupa yote mwilini, athari zinazotokea kwenye meno ya ukubwani ndio changamoto
inayopewa kipaumbele zaidi na watu wengi kwani huathiri muonekano wao mzuri wa
mhusika hivyo kumnyima uhuru sehemu nyingi anazokuwapo.
Maambukizi
Izingatiwe, kuzidi kwa madini ya floridi kupita kiasi kwenye
meno huanza kwa watoto wakiwa wadogo wenye miezi 20 mpaka 30. Halikadhalika ni muhimu kujua kuwa umri mpaka
miaka minne ya mtoto bado anakuwa katika kipindi hatarishi cha kuwa na meno
yaliyoathiriwa na madini haya katika utu uzima wake. Hata kuanzia miaka minane na kuendelea, mtoto
hawezi kuathirika tena.
Kiwango salama cha madini ya floridi kwa binadamu ni 0.05
mpaka 0.07 mg F/Kg/Kwa siku. Kiasi
chochote juu ya kiwango hiki husababisha kuongezeka kwa uwezekano wa kuwa na
meno yaliyoathirika.
Athari za kuzidi kwa madini ya floridi hivyo kuathiri rangi
ya meno zinaweza kuepukwa kwa kudhibiti kiasi cha madini ya floridi ambayo
mtoto anapewa mpaka umri usiopungua miaka sita.
Vyanzo vya floridi
Madini ya floridi hupatikana kwa wingi, japo kwa uchache,
kwenye maji tunayotumia kwa shughuli mbalimbali kama vile kunywa au kupikia,
magadi ambayo hutumika wakati wa kupika vyakula mbalimbali kama vile mrenda na
maandazi au kwenye dawa za meno tunazotumia kupigia mswaki.
Madini ya floridi ni maarufu na hujulikana sana kwa uwezo
wake wa kuzuia meno kutoboka. Kwa
ujumla, madini haya husaidia sana kuimarisha mifupa yote katika mwili wa
mwanadamu. Umuhimu wake huonekana zaidi
linapokuja suala la uimara wa meno.
Utengenezwaji wa meno, kwa kiasi kikubwa, huhusisha
muunganiko wa madini ya phosphorus na calcium ambapo kuongezeka kwa madini ya
floridi hufanya muunganiko huo kuwa mgumu zaidi kuweza kuhimili shughuli zote
zifanywazo na meno.
Kwa lugha nyepesi, kutokuwepo kwa madini haya mwilini
huyafanya meno kuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kutafuna, kung’ata au kingine
chochote kinachoweza kufanywa na meno.
Madhara ya floridi
Kila kitu kikizidi mahali kinapopaswa kutumika huwa kunakuwa
na madhara yanayojitokeza. Hata kuzidi
kwa madini ya floridi kwenye meno nako kuna matokeo kama hayo kutegemea wingi
wa madini yaliyozidi.
Kwa kutambua kigezo hicho, tunaweza kwa ajili ya kueleweka
kuyagawa katika makundi kulingana na mtazamo wa mhusika na jamii kwa ujumla.
Madhara kidogo. Kundi
hili lina watu ambao meno yao yana weupe wa chaki. Hii inaweza kujitokeza kwa jino zima au
sehemu ya jino, huenda ikawa kinywa kizima.
Wapo wenye madhara ya wastani. Hii ni kwa ile hali ambayo meno huwa na rangi
ya kahawia kwa mbali. Hii husababisha
aibu kwa baadhi ya wenye tatizo hilo kiasi cha kuwa wahanga wa kujihisi wenye
kasoro kwenye jamii.
Baadhi ya waathirika huwekwa kwenye kundi la wenye madhara
makubwa kwa kuwa ni watu ambao meno yao huweza kuvunjika ama kukatika hivyo
kuwafanya wapate ganzi ama meno husika kuwa yanauma wakati wa kula ama
kunywa. Mara nyingi kundi hili ndilo
ambalo wengi wao, meno yao huvunjika vunjika na kutokuwa na sura nzuri. Hawa wanahitaji kuwa makini zaidi ili
kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kuvunjika au kukatika kwa
meno yao.
Namna ya kuzuia hali hii ni kuepuka kutumia maji na vitu
vingine vinavyoingia mwilini ambavyo vina kiwango kikubwa cha madini ya
floridi hasa kipindi cha utotoni ambapo meno huwa yanaota.
Ikumbukwe kuwa katika umri wa miezi 20 mpaka
miezi 30 tangu mtoto kuzaliwa ndicho kipindi hatari zaidi kinachosababisha hali
hii kama mtoto atalishwa vitu vyenye madini mengi ya floridi.
No comments:
Post a Comment