Moja ya dalili za saratani za aina nyingi huambatana na
uwepo wa uvimbe wa aina mbalimbali kwenye sehemu husika ya mwili kulingana na
aina ya saratani.
Dhana hii imezua hofu kubwa kwa miongoni mwa wanawake wengi
hasa inapotokea vipimo vikagundulika wana uvimbe ulioota kwenye mifuko yao ya
uzazi.
Habari njema ni kwamba, uvimbe huo hautokani na ugonjwa wa
saratani, bali husababishwa na sababu nyinginezo kama nitakavyoeleza, ila kwa
kuwa hautokani na saratani, sio vyema kufumbia macho kwa sababu zina madhara
mengine kwenye mfumo wa uzazi na afya.
Uvimbe huo huitwa uterine fibroids kwa kitaalam, ni uvimbe
usiotokana na saratani na mara zote huwa unaota na kukua kwenye ukuta au tabaka
lililopo kwenye mfuko wa uzazi.
Uvimbe huu hutofautiana kwa ukubwa wa maumbile na wakati
mwingine ukicheleweshwa unaweza kufikia hata ukubwa wa tikiti maji.
Pia, hutofautiana kwa idadi kati ya mwanamke mmoja na
mwingine, mwanamke mmoja anaweza akaotwa na uvimbe zaidi ya mmoja kwenye mfuko
wake wa uzazi, lakini mwanamke mwingine anaweza akaotwa na uvimbe mmoja tu
kwenye mfuko wake na mara nyingi moja ya madhara yanayosababishwa na uvimbe huo
ni mkandamizo wa mfuko wa uzazi, huulazimisha kupanuka hadi kugusa kwenye
viwambo vya mbavu na hapo ndipo matatizo mengi hujitokeza.
Hata hivyo, wanawake wengi hupatwa na tatizo hilo kwenye
mifuko yao ya uzazi, lakini wengi wao hawatambui kama wanalo kwa sababu
hauoneshi dalili hadi unapokuwa mkubwa kupita kiasi na kuanza kuleta matatizo
kiafya.
Nawashauri wanawake ni vyema wakajenga utamaduni wa kupata
vipimo mara kwa mara ili kubaini ukiwa katika hatua za awali na kwa kufanya
hivyo, watajiepusha na madhara makubwa ya kiafya yasababishwayo na uvimbe huo.
Kama nilivyoeleza hapo juu, uvimbe huchukua muda hadi
kuonesha dalili zake, kama mwanamke mwenyewe hana utamaduni wa kupata vipimo
mara kwa mara; au kama utakuwa umedumu kwa muda mrefu, anaweza kuziona dalili
kama vile za hedhi iliyopitiliza ambayo baadaye inaweza kumsababishia kupata
anemia, maumivu ya mgongo na kiuno. Pia anaweza
kupata haja kubwa kwa shida, maumivu makali chini ya kitovu na hasa ikitokea
uvimbe umeshakuwa mkubwa, kupata haja ndogo mara kwa mara kuliko kawaida na
kupata maumivu makali wakati wa tendo la ndoa.
Ukiona dalili hizi, ni Dhahiri una tatizo hilo na ni vyema
kwenda hospitali kwa ajili ya vipimo na mpango wa matibabu. Uvimbe unaoota kwenye mfuko wa uzazi japo
hauwezi kusababisha saratani, lakini una madhara mengine makubwa kiafya ambayo
ni pamoja na matatizo wakati wa kujifungua yanayoweza kuhatarisha maisha ya
mama na mtoto hasa kama atakuwa alishika ujauzito akiwa tayari ana uvimbe. Lakini pia uvimbe huweza kusababisha mwanamke
kukosa uwezo wa kushika mimba, mimba kutungwa nje ya uzazi na tatizo lingine kubwa
ni mimba kuharibika mara kwa mara. Sababu
kubwa zinazochangia tatizo hili ni matatizo yanayojitokeza kwenye mfumo wa
homoni.
Kisayansi, kwenye mwili wa mwanamke kuna homoni
(vichocheo) za estrogen na progesterone, huwa zinafanya kazi ya kuchochea
maendeleo ya ukuaji wa sehemu ya ndani ya mfuko wa uzazi kwenye kila mzunguko
wa hedhi wa kila mwezi.
No comments:
Post a Comment