Februali 4 kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya
saratani. Siku hii hutumika zaidi kutoa
elimu kwa umma juu ya madhara ya maradhi hayo na namna ya kukabiliana nayo na
kauli mbiu kwa mwaka huu inasema, “Tunaweza, Ninaweza.”
Ujumbe huo umebeba dhana nzito kwani bado kuna dhana potofu
imeendelea kujengeka miongoni mwa jamii juu ya maradhi hayo yanayoendelea
kuathiri kwa kiwango kikubwa watu wengi duniani.
Tunaelezwa kuwa saratani ni miongoni mwa maradhi yanayoua
watu wengi na hapa nchini hili linashuhudiwa.
Kwani jamii imeendelea kuwatesa hasa wanawake, mbali ya
saratani ya shingo ya uzazi ipo ya matiti, na kwa wanaume saratani ya tezi
dume imeendelea kugharimu maisha ya wengi wao.
Pia ndiyo ugonjwa ambao dawa zake zina gharama kubwa na kwa
Tanzania, Serikali imeendelea kutumia mabilioni ya shilingi kukabiliana nao na
kutibu walioathirika tayari.
Wataalamu wa afya wanasema saratani si ugonjwa mmoja bali ni
mkusanyiko wa maradhi takribani 200 na kila ugonjwa ukiwa dalili zake tofauti
na njia za kuupima na kuutibu.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema viashiria vya kansa
vitaongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi cha miaka 20 ijayo.
Ugonjwa huo ni wa pili kwa kuua duniani kama ilivyoelezwa na
mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka
taasisi ya saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Chrispin Kahesa.
Anasema watu milioni 6 hufariki duniani kila mwaka kutokana
na saratani na wengi wao hutoka nchi zinazoendelea Tanzania ikiwa miongoni.
Je kwa Tanzania hali
ikoje?
Dk Kahesa anasema ORCI hupokea wagonjwa wapya wa saratani
50,000 kila mwaka huku saratani ya shingo ya kizazi ikiongoza.
Anasema saratani ya shingo ya kizazi imekuwa tishio kwa
wanawake wengi nchini. Kwani takwimu za
mwaka 2016 zinaonesha asilimia 33 ya wanawake wenye saratani, wanaugua saratani
ya shingo ya kizazi. “Wengi wao hupoteza
maisha kutokana na kushindwa kubaini uwapo wa tatizo hilo,” anasema Mkurugenzi
huyo wa Kinga na Tiba.
Anasema saratani ya shingo ya kizazi inashika nafasi ya pili
kwa maradhi ya saratani kwa wanawake na ni sababu kubwa ya vifo vyao si kwa
Tanzania tu, bali kwa nchi karibu zote zinazoendelea.
WHO inasema kama saratani hiyo haitachukuliwa hatua Zaidi,
kuna uwezekano mkubwa ifikapo 2030 wanawake takribani 430,000 watafariki dunia
kutokana na ugonjwa huo.
Kwani kidunia, kati ya vifo 275,000 asilimia 85 husababishwa
na saratani ya shingo ya kizazi.
Saratani hiyo husababishwa
na nini?
Dk Kahesa anasema saratani ya shingo ya kizazi husababishwa
na virusi vya HBV, HCV na Human papilloma Virus (HPV) vinasababishwa na
ufanyaji wa ngono na hutokea zaidi katika nchi za Jangwa la Shara. “Lakini kwa Tanzania kirusi cha HPV ndiyo
chanzo kikubwa cha maambukizi ya saratani ya shingo ya uzazi,” anasema Dk
Kahesa.
Anasema kama kinga ya mwili itashindwa kuondoa maambukizi ya
virusi hivyo, ndipo mgonjwa huugua saratani ya shingo ya kizazi.
“Kama maambukizo hayo yataendelea kwa muda mrefu, chembe hai
za kawaida huanza kukua bila mpangilio na kuwa saratani, jambo ambalo linaweza
kuchukua miaka miwili hadi ishirini tangu kuambukizwa kuja kubainika,” anasema
Dk Kahesa.
Anasema saratani nyingi wanazougua Watanzania zinasababishwa
na virusi. Anatolea mfano wa kirusi cha
HPV ambacho huenea kwa njia ya kugusana sehemu za siri.
Anasema kirusi hicho huambukiza hata kama tendo la
kujamiiana halifanyika. Ili kujikinga na
maambukizi hayo, Dk Kahesa anasisita matumizi ya mpira wa kiume ili kupunguza
maambukizi lakini si kwa asilimia 100. Dk
Kahesa anasema kwa sasa maambukizi ni makubwa hasa kwa wanwake wenye umri chini
ya miaka 25 ambao miili yao haijapambana na kupata kinga ya mwili ya kuviondoa
virusi hivyo.
Kinachochangia maambukizi
ya HPV
Baadhi ya vitu vinavyochangia maambukizi ya HPV ni kuanza
kufanya tendo la kujamiiana katika umri mdogo, upungufu wa kinga mwilini,
kurithishana kati ya vizazi na ukali wa virusi.
Dk Kahesa anasema hakuna dalili zinazojitokeza katika hatua za mwanzo za
maambukizi, lakini katika hatua za mbele za ugonjwa, dalili zinazojitokeza kama
kutokwa na damu au ute ukeni kusiko kwa kawaida, maumivu wakati wa tendo la
kujamiiana, uvimbe ukeni na kutokwa haja ndogo na kubwa kusikojulikana. Anasema upimaji wa ufasaha unawezesha
ugunduzi wa mapema na huweza kuzuia kuendelea kwa ugonjwa na hatimaye kupunguza
hatari ya vifo vitokanavyo na saratani hiyo.
Tatizo hilo linaweza
kudhibitiwaje?
Anasema njia mbili za kuapambana na tatizo hilo ni kwa
kupata chanjo dhidi ya virusi vya HPV.
Pia wanawake wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara
ili kugundua ugonjwa mapema.
Anasema tiba ya mapema ni gharama ndogo kuliko ile ya
ugonjwa ulioenea na pia huweza kuondoa kabisa saratani. Katika kukabiliana na saratani ya shingo ya
uzazi, Dk Kahesa anasema tayari wameweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wa
kike kuanzia darasa la nne nchini kote wanapatiwa chanjo itakayosaidia kuwakinga
na saratani ya shingo ya kizazi. “Wanaougua
ugonjwa huu idadi yao ni kubwa lazima tuweke mikakati ya pamoja
kuhakikisha tunapunguza idadi hiyo,
ni suala la kuamua tu kwa kuanzia na mtu mmoja mmoja, familia na mwisho kwa
Watanzania wote na baadhi ya sababu zinazosababisha ugonjwa huu tunaweza
kuzikwepa,” anasema.
Saratani ya matiti
Tofauti na maradhi mengine kama malaria ambayo dalili zake
hueleweka, saratani ya matiti hushambulia kimya kimya.
Saratani ya matiti ni miongoni mwa inayokatisha uhai wa
maelfu ya wanawake kila mwaka na ni ya pili kwa kusababisha vifo vya wanawake
duniani kutokana na kutogundulika kwa wakati.
Saratani hiyo hutokea katika titi ambalo lina sehemu ya
kutengenezea maziwa ijulikanayo kitabibu ‘Lobules na katika aina mojawapo ya
mishipa inayounganisha yanapotengenezwa maziwa na chuchu.
Saratani hiyo inapotokea husababisha kubadilika kwa ukuaji
wa chembe hai za mwili na kuwa wa kiholela pasipo kufuata utaratibu wa kawaida.
Sababu yake ni nini?
Bado sababu ya moja kwa moja inayosababisha saratani hiyo
haijagunduliwa na wanasayansi na matibabu yake wanadai bado ni fumbo. Lakini yapo mambo yanayoaminika kuchangia
tatizo hilo ikiwamo aina fulani ya chembe za urithi inayosababisha chembe
zingine zipoteze ufanisi wake.
Pia kuanza hedhi katika umri mdogo au kukoma siku katika
umri mkubwa, kutozaa kabisa na kutonyonyesha kabisa au kunyonyesha kwa muda
mfupi.
Tabia ya kutumia mafuta mengi kwenye chakula nayo ni
miongoni mwa sababu, kutofanya mazoezi ya mara kwa mara, unene kupita kiasi,
uvutaji wa sigara, utumiaji wa pombe kupita kiasi na historia ya saratani ya
matiti katika familia.
Dk Kahesa anasema saratani hiyo inaweza kuwakuta pia
wanaume.
Anasema kwa Tanzania hadi sasa ni asilimia moja tu ya
wanaume waliougua saratani ya matiti.
Matibabu ya saratani
Dk Mark Mseti mkuu wa kitengo cha Bima cha ORCI anasema
matibabu ya saratani yanategemea vitu vikubwa vitatu.
Moja ni kujua hatua ya saratani iliyofikia, hali ya ugonjwa
na ridhaa ya mgonjwa kuhusiana na aina ya matibabu anayotaka kupatiwa.
“Lakini hapa cha msingi ni muhimu kujua kuwa maradhi ya saratani
hayaambukizi na yanaweza kukaa mwilini kati ya miaka mitano hadi 10, ndipo
dalili zake huanza kujitokeza wazi,” anasema Dk Mseti. Anatoa wito kwa jamii kujitokeza hospitali
kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kama maradhi hayo yapo yaweze kutibiwa
haraka.
“Saratani inatibika, watu wawahi uchunguzi mapema. Ukiwahi unapona na utarejea kwenye maisha
yako ya kawaida,” anasema daktari huyo.
No comments:
Post a Comment