Kama ilivyo misuli ya mwili, mifupa nayo ni tishu zenye uhai
zinazofaidika kwa mazoezi ya mwili. Mazoezi huimarisha mifupa na kuifanya iwe
na nguvu, iwe na umbo zuri pamoja na ujazo mzuri.
Kwa kawaida mifupa huendelea kukua na kuwa imara katika miaka ya
utotoni hadi wakati wa ujana kabla ya miaka 30. Baada ya kipindi hiki cha umri,
mifupa taratibu inaanza kupoteza uimara wake na katika kipindi hiki ndipo
mazoezi yanapohitajika zaidi. Mazoezi yanasaidia kuimarisha misuli
inayojishikiza katika mifupa na kuwa na stamina, mambo ambayo yanapunguza
uwezekano wa mtu kuanguka ovyo na kuvunjika mifupa.
Mazoezi yanayoimarisha afya ya mifupa ni muhimu hasa kwa
wagonjwa wenye udhaifu wa mifupa, watu wanaofanya kazi za kukaa ofisini muda
mrefu, wazee na wanawake waliokoma kupata siku zao za hedhi.
Mazoezi mazuri kwa ajili ya uimara na afya ya mifupa ni yale
yanayohusu na mwili kubeba uzito.
Mifano ya mazoezi haya ni kama vile kubeba vitu vizito, kupiga
pushapu, kupanda milima, kupanda ngazi, kukimbia taratibu, kutembea kwa muda
mrefu pamoja na kucheza muziki unaohitaji minenguo ya aina mbalimbali.
Mazoezi haya pia, yanaweza kuchanganywa na mazoezi ya kuimarisha
afya ya moyo na misuli. Mazoezi kama vile kuogelea, kuruka kamba na kuendesha
baiskeli yanaweza pia kusaidia moyo na misuli kuwa na nguvu.
Kabla ya kuanza mazoezi yanayoimarisha mifupa, ni jambo la
busara kupata ushauri wa kitabibu. Jambo hili ni muhimu hasa kwa watu wenye
magonjwa ya muda mrefu kama vile udhaifu wa mifupa, maumivu ya mgongo, kisukari,
matatizo ya moyo na figo, shinikizo la damu, kifafa na unene wa kupindukia.
Watu wazima wenye miaka zaidi ya 40 ambao kwa kawaida hawana
mazoea ya kufanya, nao wanatakiwa kupata ushauri wa kitabibu kabla ya kuanza
mazoezi ya kuimarisha mifupa yao. Mazoezi ya kuimarisha mifupa sharti yafanyike
kila siku au mara tatu katika kipindi cha juma moja na yasiwe chini ya dakika
30 kwa siku.
Shirika la Afya Duniani (WHO) katika chapisho lao la mwaka 2010
linalozungumzia umuhimu wa mazoezi kwa afya (GRPAH), linapendekeza watu wenye
umri kuanzia miaka 18 na kuendelea, wafanye mazoezi mepesi angalau kwa dakika
150 au mazoezi mazito angalau kwa dakika 75 ndani ya juma moja. Ni vizuri
kusikiliza kengele ya mwili wako hasa pale unapoanza mazoezi haya.
Pale unapoanza mazoezi unaweza kuhisi maumivu ya misuli, hivyo
basi usijilazimishe kuendelea. Simamisha mara moja mazoezi yako hasa pale
unapohisi maumivu ya kifua wakati wa mazoezi na wasiliana na daktari.
Kwa watu wanajali afya ya mifupa yao, pamoja na mazoezi, ni
jambo la busara kujiepusha na matumizi ya tumbaku, ulevi wa pombe na matumizi
ya dawa za kulevya.
Inashauriwa pia kupata mlo kamili hasa wenye kiasi cha kutosha
cha madini ya kalisi (calcium) na vitamini mbalimbali. Dagaa na samaki
tunaoweza kuwatafuna na mifupa yao, korosho pamoja na kunywa maziwa kwa kiasi,
ni njia bora za kutupatia madini ya kalisi.
No comments:
Post a Comment