Tuesday, February 13, 2018

TATIZO LA MUWASHO NDANI YA KOO



Muwasho ndani ya koo unatokana na sababu mbalimbali japo kwa kiasi kikubwa unachangiwa na mzio (aleji) wa vitu ikiwamo ile itokanayo na baadhi ya vyakula.

Kupitia mzio unaotokana na vyakula, hutokea pia wakati kinga ya mwili inapambana na vimelea vilivyopo kwenye vyakula tunavyokula vyenye kuhatarisha afya zetu.

Kwa kawaida, kinga ya mwili hupambana na vimelea hivi vya maradhi muda mfupi baada ya kula vyakula vyenye vimelea vya maradhi.

Lakini kwa watu wengine, mzio unaweza kutokea hata siku kadhaa baada ya kula vyakula hivyo.

Mzio unaweza kuwa wa kawaida ukiambatana na dalili chache zikiwamo za muwasho ndani ya koo au mdomoni.

Hata hivyo, mara chache inaweza kutokea kuleta madhara makubwa zaidi kiafya.  Hivyo ni vyema kuwa makini katika ulaji wa baadhi ya vyakula kama ngano, baadhi ya aina za kunde, baadhi ya nyama mbichi, mayai na hata maziwa.

Vyote hivyo mara nyingi husababisha mzio kwa walio wengi.
Mzio hutokea pia kutokana na matumizi ya aina mbalimbali za dawa ambazo husababisha muwasho ndani ya koo.

Wengi wanaoshambuliwa na mzio unaotokana na matumizi ya dawa hasa kiantibayotiki kama vile penicillin zinazotumika kuzuia maambukizi ya vimelea mbalimbali.

Mzio huu unapotokea huleta ishara mbalimbali mwilini ikiwamo muwasho ndani ya koo.

Mtu anapokuwa na mafua makali hasa wakati wa baridi, maumivu na muwasho ndani ya koo yanaweza kuongezeka mara dufu vikiambatana na hali ya homa na maumivu ya kifua.

Muwasho huu unaweza kudumu kwa muda usipopatiwa tiba na unaweza kuwa hatari kwa afya.

Muwasho ndani ya koo pia unasababishwa sana na maambukizi ya kibakteria na yale yatokanayo na baadhi ya virusi vya maradhi mbalimbali.

Kuna maambukizi ya maradhi ambayo mara nyingi hutokea kooni ambayo kwa kitaalamu yanaitwa “streptococall” au “strep throat”.
Maambukizi haya yanapotokea yanaweza yakaambatana na vidonda kwenye koo ambavyo wengi pia huwa wanavipata (tonsillitis) yakiambatana na muwasho ndani ya koo hatimaye kuongezeka na kuleta maumivu makali kwenye koo.  Baadhi ya virusi vinavyosababisha mafua pia vinaweza kuleta muwasho ndani ya koo.

Ni Dhahiri kuwa, kila mmoja anafahamu umuhimu wa maji kwenye maisha yetu ya kila siku na hasa kwa afya.

Ukosefu wa kiwango cha kutosha cha maji unasababisha kwa kiasi kikubwa sana tatizo la muwasho ndani ya koo.  Upungufu wa maji mwilini unatokea pale ambapo mwili unapoteza kiasi kikubwa cha maji kuliko kile kinachoingia na mara nyingi hali hii hutokea wakati wa joto sana, baada ya kufanya mazoezi ya mwili au hata wakati wa homa.  Upungufu wa maji mwilini unatokea pale ambapo mwili unapoteza kiasi kikubwa cha maji kuliko kile kinachoingia na mara nyingi hali hii hutokea wakati wa joto sana, baada ya kufanya mazoezi ya mwili au hata wakati wa homa.  Upungufu wa maji mwilini unaweza kusababisha kukauka kwa mdomo, japo hali hii huwa ni ya muda kwa sababu mdomo na koo havipati mate ya kutosha kutokana na upungufu wa maji mwilini na hivyo kupelekea kupata muwasho ndani ya koo.

Utendajikazi wa madawa mwilini pia unasababisha muwasho ndani ya koo.

Baadhi ya madawa yanaweza kusababisha kikohozi kikavu na muwasho ndani ya koo ambayo hayatokani na aleji zinazotokana na dawa.  Watu wanaotumia baadhi ya dawa za shinikizo la damu wanapaswa kutambua kuwa dawa hizo zinaweza kusababisha kikohozi kikavu na muwasho ndani ya koo wakati wa utendaji kazi wake mwilini.  Kwa kawaida dalili hutokea mara tu baada ya kutumia dawa hizi na mara zote haziambatani na dalili zingine tofauti na muwasho ndani ya koo na kikohozi kikavu.

Kwa kawaida huwa si rahisi kugundua kama muwasho ndani ya koo umetokana na baadhi ya magonjwa au ile inayotokana na baadhi ya vyakula, hivyo ni vyema kuzitambua dalili zake ndipo utagundua kama muwasho huo umetokana na vyakula au maradhi mengine.

Share:

Monday, February 12, 2018

KOROSHO HUSAIDIA KUPUNGUZA UNENE


Utafiti uliofanywa kuhusu korosho, umeonesha zina faida nyingi kiafya ikiwamo tiba ya maradhi ya moyo.

Tunaelezwa ulaji wa korosho mara kwa mara husaidia kuweka sawa afya ya moyo kwa sababu licha ya kuwa na kiwango kidogo cha mafuta (fat), lakini pia zina aina ya mafuta (Monounsaturated fats) ambayo hutoa kinga kwenye moyo, aina ambayo huweza pia kupatikana kwenye Olive oil.

Utafiti unaonesha ndani ya Korosho kuna kirutubisho aina ya Oleic Acid ambacho huimarisha afya njema ya moyo na huwafaa hata wagonjwa wa kisukari.

Pia, utafiti uliochapishwa kwenye jarida la masuala ya virutubisho nchini Uingereza (British Journal of Nutrition), ulionesha watu waliopendelea kula korosho na bidhaa zake, kama butter, idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa moyo vilipungua kati asilimia 11 na 19.

Hata hivyo, utafiti huo umebainisha watu wanaotumia korosho angalau mara nne kwa wiki, wameonesha kuondokewa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo kwa asilimia 37, lakini iwapo mtu atakula sana korosho, atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuepuka kushambuliwa na magonjwa.

Korosho ni chanzo kizuri cha madini aina ya Copper ambayo ni muhimu mwilini, lakini pia ina madini yanayoimarisha kinga ya mwili na mifupa na hutatua tatizo la upungufu wa uzalishaji wa nguvu za kiume mwilini.

Faida nyingine kwa watu wanaotaka kupungua mwili, ulaji wa korosho mara mbili kwa wiki husaidia kupunguza uzito uliopitiliza, licha ya kuwa na mafuta mengi pia ni chanzo kizuri cha madini ya kopa, magnesium na Phosphorus.
Share:

JINSI YA KUMPATIA HUDUMA YA KWANZA MGONJWA WA KIFAFA


Kifafa ni ugonjwa wa ubongo unaomfanya mtu azimie.  Huenda mtu akazimia kwa dakika tano au zaidi ya hapo, lakini watafiti wanasema mtu huzimia kunapokuwa na utendaji usio wa kawaida katika chembe za ubongo.

Sasa kama hali hiyo itajitokeza, hutakiwi kushtuka, tulia na kwa haraka utafute namna ya kumsaidia mgonjwa ili kuokoa maisha yake.

Tovuti ya The Beehive inaorodhesha mambo unayopaswa kufanya kumsaidia mtu mwenye kifafa anapopatwa na ugonjwa huo.

Namna ya kumsaidia mgonjwa wa kifafa

Hatua ya kwanza mzuie taratibu, usijaribu kumzuia kwa kutumia nguvu kama kumshika mikono na miguu kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha majeraha kwa mgonjwa na pia kwa yule anayejaribu kumsaidia.

Ondoa vitu vyote vyenye ncha kali vinavyoweza kumdhuru mgonjwa.

Fungua nguo au kitu chochote kilichopo kwenye shingo ambacho kinaweza kuathiri upumuaji.

Endapo mgonjwa atazimia, weka kitu laini katika kichwa chake na umsaidie alale upande.

Usimpulizie hewa mdomoni, fanya hivyo iwapo hataweza kupumua baada ya kifafa kutulia.

Mgonjwa anapotulia na kurudiwa na fahamu zake muoneshe upendo asihisi kama ametokewa na kitu chochote kibaya.

Ikiwa mgonjwa amezimia kwa zaidi ya dakika 10 hakikisha unamuwahisha hospitali ili kuokoa maisha yake.
Share:

ATHARI ZA KISUKARI KIPINDI CHA UJAUZITO



Ugonjwa wa kisukari ni miongoni mwa maradhi sugu yanayoendelea kuathiri afya za mamilioni ya watu wa nchi nyingi duniani Tanzania ikiwamo.

Ugonjwa huo unaongezeka haraka kiasi cha kuonekana ni janga la ulimwengu.

Tunaelezwa kuwa kuna aina mbili za kisukari.  Aina ya kwanza huanzia utotoni, na madaktari hawajui jinsi ya kuizuia.  Lakini kuna aina ya pili ambayo imeathiri watu wengi kwa takribani asilimia 90 ya wanaougua ugonjwa huo.

Ingawa zamani aina ya pili ya kisukari ilihusianishwa tu na watu wazima, hivi karibuni imegundulika kuwaathiri pia watoto.

Lakini wataalamu wanasema mtu anaweza kujikinga ili asipatwe na kisukari.

Pamoja na kwamba ni tatizo kwa watu wengi wa rika na jinsia tofauti, ila kupanda kwa kiwango cha kisukari kumeweza kuwa tatizo pia kwa wajawazito kiasi cha kuwasababishia matatizo mbalimbali yeye na mtoto aliyeko tumboni.

Kisukari cha mimba kinawatokea hata wale ambao awali hawakuwahi kuugua ugonjwa huo.

Hali hiyo ikitokea humuweka mjamzito kwenye hatari ya kupata kifafa cha mimba, msongo wa mawazo pamoja na kujifungua kwa njia ya upasuaji.

Kisukari cha mimba huwakumba asilimia 3 hadi 9 ya wanawake katika ile miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito.

Huathiri asilimia moja ya wanawake waliochini ya miaka 20 na asilimia 30 ya walio juu ya miaka 44.

Asilimia 90 ya wanaokumbwa na tatizo hilo huweza kuondokana nalo baada tu ya kujifungua.

Utafiti unaonesha wanawake wenye kiwango kikubwa cha sukari kipindi cha ujauzito wapo katika hatari ya kujifungua watoto wakubwa, wenye kiwango kidogo cha sukari mwilini na wenye manjano.  Kisukari cha mimba ni hatari na kama hakitatibika, kinaweza kusababisha mtoto aliyeko tumboni kupoteza maisha.

Watoto wanaozaliwa baada ya muda kupita miezi tisa, huzaliwa wakiwa na uzito mkubwa na hupatwa na ugonjwa wa kisukari wakiwa na umri mkubwa.

Nini kinachochea kisukari cha mimba

Yapo mambo yanayochochea kisukari cha mimba ambayo ni pamoja na uzito wa kupindukia, historia ya kuwa na kisukari cha mimba katika ujauzito uliopita, historia ya ugonjwa wa kisukari hasa cha ukubwani katika familia, uvimbe katika ovari, hali inayofahamika kama polycystic ovarian syndrome, wanawake wenye umri juu ya miaka 35 wapo katika hatari.

Pia kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa katika ujauzito uliopita, matumizi ya dawa aina ya glucocorticoids na beta blockers au antipsychotics wakati wa ujauzito, huongeza hatari ya tatizo hilo, kuwa na kiwango kikubwa cha presha ya damu wakati wa ujauzito ni kichochezi pia.

Matatizo wakati wa ujauzito

Watoto wanaozaliwa na wanawake wenye kisukari cha mimba ambao hawakupatiwa matibabu, huwa na uzito mkubwa.

Lakini mjamzito aliyepatiwa matibabu ya tatizo hilo, mtoto anaweza akazaliwa mdogo ukilinganisha na miezi husika, kupatwa matatizo ya ukuaji akiwa ndani ya uzazi.

Utafiti unaonesha tatizo la kujifungua watoto wenye uzito mkubwa huwakumba wajawazito kwa asilimia 12.

Lakini wale ambao hawajawahi kuugua kisukari cha mimba wanaougua ni asilimia 20 pekee.

Hali ikoje upande wa watoto

Wale wanaozaliwa na mama zao wenye tatizo hilo, huwa katika hatari ya kuugua homa ya manjano na huwa na kiwango kidogo cha sukari, kiwango kikubwa cha chembechembe nyekundu za damu, kupatwa na matatizo katika mfumo wa hewa na kuathiri upumuaji kwa sababu ya kuzaliwa mapafu yakiwa bado machanga.

Pia huwa na kiwango kidogo cha madini ya kalisiamu pamoja na magnesium.

Mambo muhimu ya kuzingatia

Kuhudhulia kliniki mara kwa mara kutokana na maagizo ya daktari kunaweza kusaidia kulitatua tatizo hilo.

Mama anatakiwa kutunza afya yake kabla na baada ya kujifungua.
Anatakiwa ajitunze na ahakikishe kiwango chake cha sukari hakipandi kupitiliza hasa kwa wanawake wenye ugonjwa wa kisukari kabla ya ujauzito.

Wanatakiwa kuzingatia aina ya vyakula wanavyotumia, kufanya mazoezi na wazuie ongezeko la uzito.

Wanawake wenye mpango wa kubeba mimba na tayari wanaugua kisukari wanatakiwa kupata virutubisho vya folate hadi kipindi cha wiki mbili wakati wa ujauzito kusudi kuondoa hatari ya kujifungua watoto wenye matatizo kwenye mfumo wa fahamu yanayofahamika kama ‘neural tube defects’.

Kwa kuzingatia haya yote, itasaidia kuondoa matatizo kwa mama na mtoto kabla na hata baada ya kujifungua.

Share:

Friday, February 9, 2018

NAMNA YA KUTIBU MIMBA CHANGA ILIYOTOKA



Aina ya utokaji mimba itakayoelezwa ni ile ijulikanayo kama utokaji mimba usio kamili ‘incomplete abortion.’

Yawezekana mjamzito alikuwa ana tatizo la mimba kutishia kutoka lakini baadaye hali hiyo inaweza kubadilika na mimba hiyo kutokana na kuharibika, ikabakisha mabaki yaliyoharibika kwenye nyumba ya uzazi.

Hali hiyo inapojitokeza ina maana ujauzito huo umeharibika, hakuna uhai wa mimba hiyo lakini mwili nao umeshindwa kutoa mabaki yote ya kiumbe kilichopo katika nyumba ya uzazi.

Utokaji mimba usio kamili mara nyingi hutokea katika muhula wa kwanza wa ujauzito.  Sababu za utokaji mimba wa aina hiyo ni sawa na aina zingine za utokaji wa mimba changa ikiwamo ile inayotishia kutoka.

Utokaji mimba usio kamili huambatana na utokaji wa damu kwa wingi ukeni ambao si wa kawaida ukilinganisha na utokaji wa damu ya hedhi.

Mgonjwa hutokwa na damu mfululizo ikiwa na mchanganyiko wa mapande ya tishu yaliyochanganyika na damu huku ikiambatana na maumivu makali yasiyovumilika wala kupotea katika eneo la chini ya kitovu na kusambaa kiunoni.

Tabibu au daktari anayekuhudumia pale atakapochunguza atagundua mlango wa nyumba ya uzazi umefunguka huku mabaki ya kiumbe mengine yakiwa yamebaki ndani ya nyumba ya uzazi.

Wakati mwingine hali hii inapotokea inaweza kuambatana na homa, kuhisi kishiwa nguvu, kuonesha dalili za hofu au kuchanganyikiwa.

Hivyo ni vizuri pale unapoona dalili hizi, chukua hatua ya haraka kufika hospitali upate matibabu.

Matibabu yake huwa ni rahisi na ni jambo linaloruhusiwa kisheria, pale inapobainika mimba imeharibika na kutoka yote, mgonjwa atalazimika kusafishwa kwa kuzingatia maadili ya kitabibu.

Usafishaji huu una lengo la kuondoa mabaki yote yaliyopo ndani ya nyumba ya uzazi.

Uwapo wa mabaki katika nyumba ya uzazi unaweza kuzidi kusababisha damu kutoka kwa wingi na pia kuwa makaribisho ya maambukizi ya bakteria.

Mgonjwa atatakiwa amsimulie historia nzima kwa daktari ili abaini chanzo ili kusudi tatizo hilo lisijitokeze katika mimba zingine hapo baadaye.

Uchunguzi unaweza kufanyika ili kujua kama chanzo ni maambukizi ikiwamo kaswende na virusi mbalimbali vinavyochangia mimba kutoka.

Dawa za kudhibiti maumivu na dawa za antibiotiki hutolewa ili kukukinga na maambukizi ya bakteria baada ya kusafishwa.

Ni muhimu kwa mgonjwa wa tatizo hili kufikishwa katika huduma za afya zinazotambulika ikiwamo vituo vya afya vya Serikali.

Ikumbukwe kuwa matibabu ya vichochoroni yanafanyika kwa kutozingatia kanuni za kitabibu, hivyo mgonjwa anakuwa katika hatari ya kusafishwa na vifaa vyenye maambukizi ya vimelea mbalimbali ikiwamo virusi vya ukimwi.  

Share:

Thursday, February 8, 2018

SARATANI INAZIDI KUTEKETEZA MAISHA YA WANAWAKE



Februali 4 kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya saratani.  Siku hii hutumika zaidi kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya maradhi hayo na namna ya kukabiliana nayo na kauli mbiu kwa mwaka huu inasema, “Tunaweza, Ninaweza.”

Ujumbe huo umebeba dhana nzito kwani bado kuna dhana potofu imeendelea kujengeka miongoni mwa jamii juu ya maradhi hayo yanayoendelea kuathiri kwa kiwango kikubwa watu wengi duniani.
Tunaelezwa kuwa saratani ni miongoni mwa maradhi yanayoua watu wengi na hapa nchini hili linashuhudiwa.

Kwani jamii imeendelea kuwatesa hasa wanawake, mbali ya saratani ya shingo ya uzazi ipo ya matiti, na kwa wanaume saratani ya tezi dume imeendelea kugharimu maisha ya wengi wao.

Pia ndiyo ugonjwa ambao dawa zake zina gharama kubwa na kwa Tanzania, Serikali imeendelea kutumia mabilioni ya shilingi kukabiliana nao na kutibu walioathirika tayari.

Wataalamu wa afya wanasema saratani si ugonjwa mmoja bali ni mkusanyiko wa maradhi takribani 200 na kila ugonjwa ukiwa dalili zake tofauti na njia za kuupima na kuutibu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema viashiria vya kansa vitaongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi cha miaka 20 ijayo.

Ugonjwa huo ni wa pili kwa kuua duniani kama ilivyoelezwa na mkurugenzi wa  Idara ya Kinga kutoka taasisi ya saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Chrispin Kahesa.

Anasema watu milioni 6 hufariki duniani kila mwaka kutokana na saratani na wengi wao hutoka nchi zinazoendelea Tanzania ikiwa miongoni.

Je kwa Tanzania hali ikoje?

Dk Kahesa anasema ORCI hupokea wagonjwa wapya wa saratani 50,000 kila mwaka huku saratani ya shingo ya kizazi ikiongoza.

Anasema saratani ya shingo ya kizazi imekuwa tishio kwa wanawake wengi nchini.  Kwani takwimu za mwaka 2016 zinaonesha asilimia 33 ya wanawake wenye saratani, wanaugua saratani ya shingo ya kizazi.  “Wengi wao hupoteza maisha kutokana na kushindwa kubaini uwapo wa tatizo hilo,” anasema Mkurugenzi huyo wa Kinga na Tiba.

Anasema saratani ya shingo ya kizazi inashika nafasi ya pili kwa maradhi ya saratani kwa wanawake na ni sababu kubwa ya vifo vyao si kwa Tanzania tu, bali kwa nchi karibu zote zinazoendelea.
WHO inasema kama saratani hiyo haitachukuliwa hatua Zaidi, kuna uwezekano mkubwa ifikapo 2030 wanawake takribani 430,000 watafariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Kwani kidunia, kati ya vifo 275,000 asilimia 85 husababishwa na saratani ya shingo ya kizazi.

Saratani hiyo husababishwa na nini?

Dk Kahesa anasema saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na virusi vya HBV, HCV na Human papilloma Virus (HPV) vinasababishwa na ufanyaji wa ngono na hutokea zaidi katika nchi za Jangwa la Shara.  “Lakini kwa Tanzania kirusi cha HPV ndiyo chanzo kikubwa cha maambukizi ya saratani ya shingo ya uzazi,” anasema Dk Kahesa.

Anasema kama kinga ya mwili itashindwa kuondoa maambukizi ya virusi hivyo, ndipo mgonjwa huugua saratani ya shingo ya kizazi.

“Kama maambukizo hayo yataendelea kwa muda mrefu, chembe hai za kawaida huanza kukua bila mpangilio na kuwa saratani, jambo ambalo linaweza kuchukua miaka miwili hadi ishirini tangu kuambukizwa kuja kubainika,” anasema Dk Kahesa.

Anasema saratani nyingi wanazougua Watanzania zinasababishwa na virusi.  Anatolea mfano wa kirusi cha HPV ambacho huenea kwa njia ya kugusana sehemu za siri.

Anasema kirusi hicho huambukiza hata kama tendo la kujamiiana halifanyika.  Ili kujikinga na maambukizi hayo, Dk Kahesa anasisita matumizi ya mpira wa kiume ili kupunguza maambukizi lakini si kwa asilimia 100.  Dk Kahesa anasema kwa sasa maambukizi ni makubwa hasa kwa wanwake wenye umri chini ya miaka 25 ambao miili yao haijapambana na kupata kinga ya mwili ya kuviondoa virusi hivyo.

Kinachochangia maambukizi ya HPV

Baadhi ya vitu vinavyochangia maambukizi ya HPV ni kuanza kufanya tendo la kujamiiana katika umri mdogo, upungufu wa kinga mwilini, kurithishana kati ya vizazi na ukali wa virusi.  Dk Kahesa anasema hakuna dalili zinazojitokeza katika hatua za mwanzo za maambukizi, lakini katika hatua za mbele za ugonjwa, dalili zinazojitokeza kama kutokwa na damu au ute ukeni kusiko kwa kawaida, maumivu wakati wa tendo la kujamiiana, uvimbe ukeni na kutokwa haja ndogo na kubwa kusikojulikana.  Anasema upimaji wa ufasaha unawezesha ugunduzi wa mapema na huweza kuzuia kuendelea kwa ugonjwa na hatimaye kupunguza hatari ya vifo vitokanavyo na saratani hiyo.

Tatizo hilo linaweza kudhibitiwaje?

Anasema njia mbili za kuapambana na tatizo hilo ni kwa kupata chanjo dhidi ya virusi vya HPV.

Pia wanawake wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kugundua ugonjwa mapema.

Anasema tiba ya mapema ni gharama ndogo kuliko ile ya ugonjwa ulioenea na pia huweza kuondoa kabisa saratani.  Katika kukabiliana na saratani ya shingo ya uzazi, Dk Kahesa anasema tayari wameweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wa kike kuanzia darasa la nne nchini kote wanapatiwa chanjo itakayosaidia kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi.  “Wanaougua ugonjwa huu idadi yao ni kubwa lazima tuweke mikakati ya pamoja kuhakikisha  tunapunguza idadi hiyo, ni suala la kuamua tu kwa kuanzia na mtu mmoja mmoja, familia na mwisho kwa Watanzania wote na baadhi ya sababu zinazosababisha ugonjwa huu tunaweza kuzikwepa,” anasema.

Saratani ya matiti

Tofauti na maradhi mengine kama malaria ambayo dalili zake hueleweka, saratani ya matiti hushambulia kimya kimya.

Saratani ya matiti ni miongoni mwa inayokatisha uhai wa maelfu ya wanawake kila mwaka na ni ya pili kwa kusababisha vifo vya wanawake duniani kutokana na kutogundulika kwa wakati.

Saratani hiyo hutokea katika titi ambalo lina sehemu ya kutengenezea maziwa ijulikanayo kitabibu ‘Lobules na katika aina mojawapo ya mishipa inayounganisha yanapotengenezwa maziwa na chuchu.

Saratani hiyo inapotokea husababisha kubadilika kwa ukuaji wa chembe hai za mwili na kuwa wa kiholela pasipo kufuata utaratibu wa kawaida.

Sababu yake ni nini?

Bado sababu ya moja kwa moja inayosababisha saratani hiyo haijagunduliwa na wanasayansi na matibabu yake wanadai bado ni fumbo.  Lakini yapo mambo yanayoaminika kuchangia tatizo hilo ikiwamo aina fulani ya chembe za urithi inayosababisha chembe zingine zipoteze ufanisi wake.

Pia kuanza hedhi katika umri mdogo au kukoma siku katika umri mkubwa, kutozaa kabisa na kutonyonyesha kabisa au kunyonyesha kwa muda mfupi.

Tabia ya kutumia mafuta mengi kwenye chakula nayo ni miongoni mwa sababu, kutofanya mazoezi ya mara kwa mara, unene kupita kiasi, uvutaji wa sigara, utumiaji wa pombe kupita kiasi na historia ya saratani ya matiti katika familia.

Dk Kahesa anasema saratani hiyo inaweza kuwakuta pia wanaume.
Anasema kwa Tanzania hadi sasa ni asilimia moja tu ya wanaume waliougua saratani ya matiti.

Matibabu ya saratani

Dk Mark Mseti mkuu wa kitengo cha Bima cha ORCI anasema matibabu ya saratani yanategemea vitu vikubwa vitatu.

Moja ni kujua hatua ya saratani iliyofikia, hali ya ugonjwa na ridhaa ya mgonjwa kuhusiana na aina ya matibabu anayotaka kupatiwa.

“Lakini hapa cha msingi ni muhimu kujua kuwa maradhi ya saratani hayaambukizi na yanaweza kukaa mwilini kati ya miaka mitano hadi 10, ndipo dalili zake huanza kujitokeza wazi,” anasema Dk Mseti.  Anatoa wito kwa jamii kujitokeza hospitali kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kama maradhi hayo yapo yaweze kutibiwa haraka.

“Saratani inatibika, watu wawahi uchunguzi mapema.  Ukiwahi unapona na utarejea kwenye maisha yako ya kawaida,” anasema daktari huyo.

Share:

Tuesday, January 9, 2018

SIO KILA UVIMBE KWENYE MFUKO WA UZAZI NI SARATANI


Moja ya dalili za saratani za aina nyingi huambatana na uwepo wa uvimbe wa aina mbalimbali kwenye sehemu husika ya mwili kulingana na aina ya saratani.

Dhana hii imezua hofu kubwa kwa miongoni mwa wanawake wengi hasa inapotokea vipimo vikagundulika wana uvimbe ulioota kwenye mifuko yao ya uzazi.

Habari njema ni kwamba, uvimbe huo hautokani na ugonjwa wa saratani, bali husababishwa na sababu nyinginezo kama nitakavyoeleza, ila kwa kuwa hautokani na saratani, sio vyema kufumbia macho kwa sababu zina madhara mengine kwenye mfumo wa uzazi na afya.

Uvimbe huo huitwa uterine fibroids kwa kitaalam, ni uvimbe usiotokana na saratani na mara zote huwa unaota na kukua kwenye ukuta au tabaka lililopo kwenye mfuko wa uzazi.

Uvimbe huu hutofautiana kwa ukubwa wa maumbile na wakati mwingine ukicheleweshwa unaweza kufikia hata ukubwa wa tikiti maji.

Pia, hutofautiana kwa idadi kati ya mwanamke mmoja na mwingine, mwanamke mmoja anaweza akaotwa na uvimbe zaidi ya mmoja kwenye mfuko wake wa uzazi, lakini mwanamke mwingine anaweza akaotwa na uvimbe mmoja tu kwenye mfuko wake na mara nyingi moja ya madhara yanayosababishwa na uvimbe huo ni mkandamizo wa mfuko wa uzazi, huulazimisha kupanuka hadi kugusa kwenye viwambo vya mbavu na hapo ndipo matatizo mengi hujitokeza.

Hata hivyo, wanawake wengi hupatwa na tatizo hilo kwenye mifuko yao ya uzazi, lakini wengi wao hawatambui kama wanalo kwa sababu hauoneshi dalili hadi unapokuwa mkubwa kupita kiasi na kuanza kuleta matatizo kiafya.

Nawashauri wanawake ni vyema wakajenga utamaduni wa kupata vipimo mara kwa mara ili kubaini ukiwa katika hatua za awali na kwa kufanya hivyo, watajiepusha na madhara makubwa ya kiafya yasababishwayo na uvimbe huo.

Kama nilivyoeleza hapo juu, uvimbe huchukua muda hadi kuonesha dalili zake, kama mwanamke mwenyewe hana utamaduni wa kupata vipimo mara kwa mara; au kama utakuwa umedumu kwa muda mrefu, anaweza kuziona dalili kama vile za hedhi iliyopitiliza ambayo baadaye inaweza kumsababishia kupata anemia, maumivu ya mgongo na kiuno.  Pia anaweza kupata haja kubwa kwa shida, maumivu makali chini ya kitovu na hasa ikitokea uvimbe umeshakuwa mkubwa, kupata haja ndogo mara kwa mara kuliko kawaida na kupata maumivu makali wakati wa tendo la ndoa.

Ukiona dalili hizi, ni Dhahiri una tatizo hilo na ni vyema kwenda hospitali kwa ajili ya vipimo na mpango wa matibabu.  Uvimbe unaoota kwenye mfuko wa uzazi japo hauwezi kusababisha saratani, lakini una madhara mengine makubwa kiafya ambayo ni pamoja na matatizo wakati wa kujifungua yanayoweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto hasa kama atakuwa alishika ujauzito akiwa tayari ana uvimbe.  Lakini pia uvimbe huweza kusababisha mwanamke kukosa uwezo wa kushika mimba, mimba kutungwa nje ya uzazi na tatizo lingine kubwa ni mimba kuharibika mara kwa mara.  Sababu kubwa zinazochangia tatizo hili ni matatizo yanayojitokeza kwenye mfumo wa homoni.

Kisayansi, kwenye mwili wa mwanamke kuna homoni (vichocheo) za estrogen na progesterone, huwa zinafanya kazi ya kuchochea maendeleo ya ukuaji wa sehemu ya ndani ya mfuko wa uzazi kwenye kila mzunguko wa hedhi wa kila mwezi.
Share: